Ofisa mdhamini wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Ali Mohammed Dadi amesema mshindi wa uwakilishi katika Jimbo la Ziwani ni Suleiman Ali wa CCM na si Asaa Hamad wa UPDP aliyetangazwa awali.
Dadi kutoka
ofisi ndogo ya Pemba alisema jana kuwa msimamizi wa uchaguzi katika
Wilaya ya Chakechake, Othman Hamisi alikosea wakati wa kujaza karatasi
ya matokeo ya mshindi wa jimbo hilo.
“Nimezungumza naye na
amesema kwamba alitoa ufafanuzi kuwa walifanya makosa katika kuandika
matokeo, hivyo aliyeshinda ni mgombea wa CCM,” alisema.
Katika
karatasi hiyo ya matokeo iliyokuwa imebandikwa ukutani, Asaa Ali Hamad
alionekana kuwa amepata kura 221 dhidi ya 121 za mgombea wa CCM, lakini
kwa ufafanuzi huo wa ZEC hakuna chama cha upinzani kilichoshinda nafasi
ya uwakilishi au udiwani.
Kwa matokeo hayo, CCM imeshinda
majimbo yote ya uwakilishi Unguja na Pemba na hivyo kuzidisha utata kwa
Rais mteule, Dk Ali Mohamed Shein anayeapishwa leo, kuunda Serikali ya
Umoja wa Kitaifa (SUK) kwa mujibu wa ibara ya 9 (3) ya Katiba ya
Zanzibar ya mwaka 1984 toleo la 2010.
Awali, kulikuwa na
uwezekano wa UPDP kutoa mteule wa nafasi ya makamu wa kwanza wa Rais kwa
kuwa kilitangazwa kimakosa kupata kiti cha uwakilishi baada ya CCM
lakini baada ya ufafanuzi huo wa ZEC matumaini hayo yameyeyuka.
Kuyeyuka
kwa ndoto hiyo ya UPDP kunamaanisha kwamba hakuna chama kilichoshika
nafasi ya pili kwa kupata kura asilimia 10 au zaidi, ambacho kwa mujibu
wa Katiba hiyo kingekuwa na nafasi ya moja kwa moja kutoa makamu wa
kwanza wa rais na baadaye mawaziri wa upinzani kuunda SUK.
Tangu Dk
Shein atangazwe kushinda urais katika uchaguzi wa marudio baada ya
matokeo ya ule wa awali kufutwa, mjadala mkubwa kwenye vyombo vya habari
na mitandao ya kijamii umekuwa ni jinsi gani atateua Serikali yake
kukidhi matakwa ya Katiba ya kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili
kuendeleza maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa baina ya CCM na CUF kabla
ya uchaguzi wa 2010.
Wakati Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar,
Vuai Ali Vuai akisema Rais Shein atatumia busara zake kumpata makamu wa
kwanza wa rais, baadhi ya wanasheria wamesema hawaoni ufumbuzi wa moja
kwa moja kutokana na upungufu huo wa kikatiba.
Kwa
mujibu wa katiba ya Zanzibar, Rais atateua makamu wa kwanza wa Rais
kutoka chama kilichoshika nafasi ya pili na mgombea wake wa urais kupata
asilimia 10 ya kura za urais, au nafasi ya makamu wa kwanza itaenda kwa
chama chochote cha upinzani kilichoshika nafaso pili kwa wingi wa viti
vya majimbo katika Baraza la Wawakilishi.
0 comments:
Post a Comment