Kiwanda
cha Saruji Tanga (Simba Cement), kimeingia makubaliano na Shirika la
Reli Tanzania (TRL), kusafirisha shehena ya saruji kwa njia ya reli
kutoka mkoani Tanga kwenda mikoa ya Mwanza na Kigoma.
Chini
ya Makubaliano hayo zaidi ya tani laki nne na nusu zitasafirishwa kwa
mwaka na hivyo kupunguza gharama ya bei ya Saruji katika mikoa ya Kanda
ya Ziwa na Magharibi kutokana na usafirishaji wa reli kuwa wa bei nafuu.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema katika
mkataba huo TRL litapata zaidi ya shilingi Bilioni 40 na hivyo kufufua
huduma ya usafirishaji wa mizigo katika reli ya kati na kuongeza mapato
kwa nchi.
Prof.
Mbarawa amewataka wafanyabiashara nchini kuanza kutumia reli
kusafirisha bidhaa zao, kwani usafiri huo ni salama na nafuu na
unachukua shehena kubwa kwa wakati mmoja.
“Asilimia
95 ya mizigo hapa nchini inasafirishwa kwa barabara hivyo mkakati wa
Serikali wa kufufua viwanda utafanikiwa kwa haraka endapo wasafirishaji
watatumia njia ya reli “, amesema Prof. Mbarawa.
Aidha,
amefafanua kuwa usafirishaji wa reli ukiimarika utapunguza ajali za
barabarani zinazosababishwa na malori na kupunguza kasi ya uharibifu wa
barabara unaotokea sasa kutokana na maroli kuzidisha uzito.
Prof.
Mbarawa amewataka watumishi wa TRL na wananchi kulinda miundombinu ya
reli na kutumia fursa ya usafiri huo kujiongezea mapato.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Bw. Martine Shigela amesema usafirishaji wa
mizigo kwa njia ya reli utatoa fursa za ajira na kuwezesha bandari ya
Tanga kupata shehena kubwa ya mizigo na hivyo kurudisha hadhi ya Mkoa wa
Tanga.
“Tanga
tuna reli, barabara na bandari hivyo tukio la kuanza kusafirisha mizigo
kwa njia ya reli itaongeza shehena kubwa katika bandari ,itatengeneza
ajira kwa wakazi wa Tanga na kukuza uchumi wa mkoa”, amesema Bw.
Shigela.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli (TRL) Bw. Masanja
Kadogosa amesema kusainiwa kwa mkataba huo kutawezesha TRL kusafirisha
tani elfu thelathini na tano za Saruji kati ya tani laki moja na elfu
tano zinazozalishwa na kiwanda hicho.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Kiwanda cha Saruji Tanga Bw. Reinhart Swart, amesema
usafirishaji wa Saruji kwa njia ya reli utaongeza kasi ya usafirishaji
wa saruji na kuwezesha kuwafikia watumiaji kwa bei nafuu.
Kiwanda
cha Saruji Tanga kinakuwa kiwanda cha kwanza kuingia mkataba na TRL
kusafirisha shehena ya mizigo tangu Serikali kuanza mikakati yake ya
kufufua reli na kupunguza usafirishaji wa shehena kubwa kwa njia ya
barabara na hivyo kuzuia uharibifu wa barabara na kupunguza ajali.
0 comments:
Post a Comment