Wanamichezo kutoka Mkoa wa Mtwara wakiingia kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona kushiriki katika Ufunguzi
wa Michezo ya UMISETA uliofanywa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Juni
10, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana
na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Selemani Jafo wakati
alipowasili kwenye uwanja wa Ndege wa Mtwara kufungua michezo ya UMISETA
kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, Juni 10, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia
wanamichezo wakati alipowasili kwenye uwanja wa Nangwada Sijaona mjini
Mtwara kufungua Mashindano ya UMISETA, Juni 10, 2019. Wengine Pichani
kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelsius Byakanwa, Waziri wa
Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa Joyce Ndalichako, na Naibu Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza,
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana
na wachezaji wa timu ya soka mkoa wa Tanga wakati alipofungua
mashindano ya UMISETA kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara
Juni 10, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika
picha ya pamoja na wachezaji wa timu ya soka ya mkoa wa Mtwara wakati
alipofungua mshindano ya UMISETA kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona
mjini Tanga Juni 10, 2019 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………………
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagizahalmashauri zote za majiji na
miji zihakikishe kuwa kuanzia sasazinatenga maeneo ya michezo na
burudani kila zinapopima viwanja.
“Naagiza kuanzia sasa, maeneo yote yanayopimwa na halmashauri na
miji yote nchini, lazima yazingatie uwepo wa maeneo ya michezo na
burudani,” amesisitiza Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Juni 10, 2019)wakati
akifungua mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa shule za msingi
na sekondari Tanzania, katika Uwanja waNangwanda Sijaona mkoani Mtwara.
Zaidi ya wanafunzi 5,400 wanashiriki mashindano hayo.
Pia, amezitaka Halmashauri ziweke mpango madhubuti wa kuyaendeleza
maeneo ya michezo na burudani sambamba na miundombinu inayozingatia
mahitaji ya wote bila kubagua.
Amesema katika baadhi ya maeneo kumekuwepo na uhaba wa viwanja vya
michezo kwa sababu ya mipango miji isiyozingatia mipango endelevu ya
sekta mbalimbali.
Hivyo, Waziri Mkuu ameagiza yafanyike marekebisho na hatua za haraka
ili kutoa fursa ya ukuaji wa michezo na kusaidia wananchi kushiriki
michezo, mazoezi na kupata burudani.
Amesema ifikapo Septemba 30, 2019, kila halmashauri iwe imefanya
mapitio ya maeneo yote yaliyokuwa yamepimwa kwa matumizi ya huduma
maalum ikiwemo michezo, burudani, shule na ibada na kutoa taarifa kama
yanatumika kwa ajili hiyo au vinginevyo.
Wakati huo huo,Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia irudishe na iimarishe mchepuo wa Elimu kwa
Michezo Chuo cha Ualimu Butimba ili kupata wataalam zaidi.
“Halmashauri ziendelee kuwaruhusu walimu mbalimbali nchini
kuhudhuria mafunzo ya michezo katika chuo cha Mendeleo ya Michezo Malya
ili kupunguza uhaba wa watalaam wa michezo katika shule mbalimbali na
nchini kwa ujumla.”
Waziri Mkuu amesema michezo ni muhimu kwa wanafunzi kwa kuwa
itawaepusha vijana na makundi yasiyofaa yakiwemo matumizi ya dawa za
kulevya na vitendo vingine visivyoendana na maadili ya Kitanzania.
Amesema michezo itawawezesha vijana kuwa na afya bora na kufanya
vema katika masomo yao kwa kuwa ili waweze kusoma vema ni sharti afya
zao ziwe njema. Pia sanaa itasaidia katika kuutambulisha utamaduni wetu
ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu.
“Kwa hiyo, ni vema tukatambua kuwa michezo na sanaa ni sehemu ya
elimu bora. Hivyo, ni muhimu kutekeleza dhana ya elimu ya michezo ili
tuweze kufikia maendeleo tarajiwa.”
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema sambamba na michezo iliyozoeleka,
pia wanaweza kuibua michezo yao ya asili ambayo itautambulisha utamaduni
wetu. “Nitoe wito kwa shule zetu, ziendeleze ubunifu wa kuibua vipaji
vya sanaa na michezo ya asili katika maeneo yetu kwa lengo la kuenzi
utamaduni wetu.”
Akizungumzia kuhusu mashindano ya mwaka huu ambayo
yameshirikisha wanafunzi wengi zaidi wenye mahitaji maalumu, Waziri Mkuu
amesema waendelee kuwahusisha wanafunzi wote katika michezo, sanaa na
burudani bila kujali aina ya ulemavu walionao.
Amesema jambo hilo ni muhimu kwa kuwa vipaji vipo kwa wote na fursa ndizo zitakazowawezesha kuonesha vipaji hivyo na kuvikuza.
Waziri Mkuu amewasisitiza wadau wote wa shule za msingi, sekondari,
vyuo, sehemu za kazi na wizara, waweke mipango ya kudumu ya
kuwashirikisha watu wenye mahitaji maalumu katika shughuli mbalimbali za
kijamii na kiuchumi bila ubaguzi wowote.
“Hakikisheni baadhi ya vikwazo katika kushirikisha watu wenye
mahitaji maalumu kwenye michezo vinaondolewa. Vikwazo hivyo ni pamoja na
kutokuwepo kwa mipango endelevu katika maeneo mbalimbali na uwepo wa
mitazamo hasi ya baadhi ya walimu, wazazi na viongozi katika maeneo yao
dhidi ya uwezo wa wanafunzi wenye mahitaji maalum.”
Aidha, Waziri Mkuu ametuamia fursa hiyo kuupongeza Mkoa wa Simiyu
kwa kuwa mmoja kati ya Mikoa ya mfano katika kutekeleza agizo lake la
mwaka jana alilolitoa kupitia michezo hiyo la kuanzishwa kwa shule
maalumu za michezo.
Mkoa wa Simiyu umejenga Shule ya Sekondari itakayokuwa kituo cha
kukuza vipaji vya wanafunzi katika michezo. “Naagiza mwakani wanafunzi
wote walioonesha vipaji katika michezo watakaofaulu Mtihani wa Elimu ya
Msingi wapangwe katika shule hiyo ili wakakuze vipaji vyao.”
Amesema bila ya kuwa na mipango ya kulea na kukuza vipaji kutoka
ngazi za chini Taifa haliwezi kupata mafanikio katika michezo nchini.
Kwani katika kipindi ambapo michezo hiyo ilisitishwa kiwango cha michezo
ya aina mbalimbali kilikuwa chini sana.
“Tangu tumerejesha shughuli za michezo katika shule zetu tumekuwa na
mafanikio makubwa sana ikiwemo kupata wachezaji wanaofuzu kucheza soka
la kulipwa kwenye viwango vya kimataifa kama Mbwana Samatta (Genk
–Belgium), Simon Msuva (Difaa El Jadid – Morocco), “
Wengine ni Shiza Kichuya (Enppi –Misri), Thomas Ulimwengu (JS Saoura
– Algeria), Hamid Mao (Petrojet – Misri), Adi Yusuph (Blackpool
–England), Hassan Kessy (Nkana – Zambia), Yahya Zaydi (Ismaily –Misri),
Shabani Chilunda, (Tenerife – Hispania) Rashid Mandawa (BDF- Botswana),
Farid Mussa ( Tenerife– Hispania).
Waziri Mkuu amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana, jitihada
zaidi zinahitajika ili kuwa na maendeleo ya kutosha katika shughuli za
michezo nchini.
Hivyo, Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na
Ofisi ya Rais TAMISEMI wakamilishe tathmini ya shule 56 za Serikali
zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kuendeleza vipaji vya michezo.
Ufunguzi huo umehudhuriwa na Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI, Selemani
Jafo, Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako,
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza,
Maafisa Elimu kutoka mikoa yote nchini, walimu wa michezo pamoja na
Maofisa wengine wa Serikali.
0 comments:
Post a Comment