Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi
Kigwangalla akizungumza na wananchi wa Kata ya Alaitole ndani ya
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro alipofika kutatua mgogoro wa wananchi
wa Kata hiyo kuzuiwa kujenga shule ya Wasichana ya bweni na Mamlaka ya
Hifadhi ya Ngorongoro katika eneo la Esere, wilayani Ngorongoro. Hata
hivyo Waziri Kigwangalla ameumaliza mgogoro huo kwa kuagiza wakazi hao
wapewe kibali cha ujenzi na mamlaka hiyo katika eneo lililopendekezwa.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi
Kigwangalla (kushoto) akisikiliza maoni na hoja za wananchi wa Kata ya
Alaitole alipofika kutatua mgogoro wa wananchi wa Kata hiyo kuzuiwa
kujenga shule ya Wasichana ya bweni na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
katika eneo lao la Esere, wilayani Ngorongoro jijini Arusha.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia na Mbunge wa jimbo la Ngorongoro Mhe.William Ole Nasha
akizungumza na wakazi wa Kata ya Alaitole iliyo ndani ya Eneo la Mamlaka
ya Hifadhi ya Ngorongoro ambayo ilizuiwa kujenga shule ya bweni ya
wasichana na mamlaka hiyo zuio ambalo limeondolewa na Waziri wa
Maliasili na Utalii aliyefika katika kata hiyo kutatua mgogoro huo.
Mkutano wa Waziri wa Maliasili na Utalii
Dkt. Hamisi Kigwangalla na wananchi wa Kata ya Alaitole katika Mamlaka
ya Hifadhi ya Ngorongoro. Mhe. Kigwangalla alifika kutatua mgogoro
uliohusisha wananchi wa Kata hiyo kuzuiwa kujenga shule ya Wasichana ya
bweni na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi
Kigwangalla akizungumza na wananchi wa Kata ya Alaitole ndani ya
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro mara baada ya kupitishwa na katika eneo
lilipoonekana fuvu linalosadikiwa kuwa ni la binadamu wa kale ambalo
bado taarifa zake zinaendelea kufanyiwa utafiti katika eneo la Esere,
wilayani Ngorongoro.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi
Kigwangalla akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Ngorongoro Mhe.William Ole
Nasha na askari wa uhifadhi wakiangalia eneo itakapojengwa shule ya
wasichana ya bweni ya kata ya Alaitole.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi
Kigwangalla, viongozi na wananchi wa Kata Alaitole wakitazama eneo
lilipoonekana fuvu linalosadikiwa kuwa ni la binadamu wa kale
lililogunduliwa na wakazi hao katika eneo la Esere, wilayani Ngorongoro.
Taarifa kuhusu fuvu hilo zinaendelea kufanyiwa utafiti na watalaam.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi
Kigwangalla akisalimiana kwa furaha na wananchi wa Kata ya Alaitole
ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro alipofika kutatua mgogoro wa
wananchi wa Kata hiyo kuzuiwa kujenga shule ya Wasichana ya bweni na
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro katika eneo la Esere, wilayani
Ngorongoro. PICHA/ Wizara ya Maliasili na Utalii.
……………………
WMU – Ngorongoro, ARUSHA.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.
Hamisi Kigwangalla, ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro uwaruhusu wananchi wa Kata ya Alaitole wajenge shule ya
wasichana ya bweni katika eneo la Esere lililo ndani ya Mamlaka hiyo ili
waweze kupata elimu kufuatia wananchi hao kuzuiwa kwa muda mrefu
kutekeleza mradi huo.
Aidha, ameutaka uongozi wa Mamlaka hiyo
utoe kibali cha kuwawezesha wananchi kata hiyo kuanza ujenzi haraka
iwezekanavyo ili fedha zilizotolewa na Serikali shilingi milioni 298
zianze kutumika.
Dkt. Kigwangalla ametoa maagizo hayo
alipokuwa akizungumza na kusikiliza kero za wananchi wa Kata Alaitole
wilayani Ngorongoro kwenye mkutano wa hadhara uliowashirikisha viongozi
wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, viongozi serikali wa kata hiyo,
viongozi wa mila wa kabila la Masai na madiwani na Mbunge wa jimbo la
Ngorongoro Mhe. William Ole Nasha.
Amesema Serikali inaunga mkono juhudi
zote za wananchi za kujiletea maendeleo akifafanua kwamba hatua ya
wananchi hao kuamua kujenga shule ya Sekondari ya Bweni ni jambo la
linalopaswa kupongezwa na kila mpenda maendeleo.
“Mnacho kitaka kiko wazi, mnataka
maendeleo ya watoto wenu, katika hili mmesema kila baba anatoa elfu
hamsini na wanawake wanatoa elfu ishirini, hili ni jambo kubwa achilia
mbali nguvu kazi mnayojitolea na tayari serikali imeshaleta milioni 298,
haiingii akilini eneo linalochangia kuleta na kuingiza mapato mengi
Serikalini kiasi cha bilioni 126 likose shule” Amesisitiza Dkt.
Kigwangalla.
Dkt. Kigwangalla ameeleza kuwa ujenzi
shule hiyo utawaondolea wanafunzi adha ya kutembea umbali mrefu
akibainisha kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono wananchi hao kwenye
mipango yao ya utekelezaji miradi ya maendeleo.
Amesema jamii hiyo pamoja na mazingira
wanayoishi kuwa ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro wanahitaji elimu. Aidha,
amesema pia ni muhimu katika sekta ya utalii kupitia utamaduni wao
akiongeza kuwa kazi ya Wizara ni kuona mafanikio ya sekta ya utalii
yanakuwa kwa kuongeza mapato na sio migogoro.
Dkt. Kigwangalla amesema Hifadhi ya
Ngorongoro ni hifadhi mseto inayoruhusu binadamu na wanyama kuwepo
katika eneo moja na kwamba hiyo ipo kwa mujibu wa sheria akiitaka
Mamlaka hiyo kuyatazama vizuri majukumu yake ya kuendeleza Utalii,
Kulinda rasilimali zililizopo kwa maana ya kuhifadhi na kuhudumia jamii
iliyo ndani ya hifadhi hiyo.
Katika hatua nyingine ameutaka uongozi wa
Mamlaka hiyo uendelee kufanya mazungumzo na wananchi hao badala ya
kujielekeza katika matumizi ya nguvu ili kupata uelewa wa pamoja
akitolea mfano wa eneo la Loliondo ambalo hivi sasa lina utulivu.
“ Viongozi wa Mamlaka mnalo jukumu la
kuwasikiliza wananchi na kuamua kwa pamoja, eneo la Ngorongoro ni Urithi
wa dunia na litaendelea kuwa hivyo kwa kuheshimu na maslahi ya Taifa na
maslahi ya walio walio wengi” Amesisitiza Dkt. Kigwangalla.
Kuhusu mahusiano baina ya wananchi na
wahifdhi Dkt. Kigwangalla amesema kuwa kupitia mkutano wake na wananchi
amebaini kuwepo kwa tatizo la mawasiliano na mahusiano baina ya wananchi
wa eneo hilo na watumishi wa Serikali walio chini ya Mamlaka ya
Hifadhi ya Ngorongoro akibainisha kwamba tayari serikali imeliona jambo
hilo na inaendelea kulifanyia kazi.
Naye Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Ngorongoro Mhe. William Ole
Nasha akizungumza wakati wa mkutano huo amempongeza na kumshukuru Waziri
wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla kwa kazi kubwa
anayoifanya ya kuhakikisha ulinzi wa rasilimali za Taifa katika maeneo
mbalimbali nchini.
Amemwomba aeendelee kutembelea maeneo
mengine ya jimbo hilo kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi wa kata
za wilaya hiyo kwa lengo la kudumisha mahusiano mema.
Mhe. Ole Nasha ameeleza kuwa hatua ya
Wizara kutafutia ufumbuzi mgogoro huo wa ujenzi wa shule ya wasichana ya
bweni, vile vile uamuzi wa serikali kutoa eneo na fedha kiasi cha
shilingi milioni 298 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo katika eneo
lililokubaliwa ni ishara tosha kwamba Serikali inawalinda na kuwajali
wananchi wake.
Amesema wananchi wa jimbo la Ngorongoro
pamoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili wako ni wasikivu na wako
tayari muda wote kushirikiana na Serikali ikiwemo ulinzi wa rasilimali
zilizopo na kuendeleza uhifadhi katika hifadhi ya Ngorongoro.
Kwa upande wao wananchi wa Kata ya
Alaitole wakizungumza kwa nyakati tofauti wamemshukuru Dkt. Kigwangalla
kwa kuamua kuwafuata na kuzungumza nao katika makazi yao wakimpongeza
kwa juhudi zake za kutatua changamoto mbalimbali kwa maslahi ya wananchi
na uhifadhi.
Aidha, wamemwomba kuendelea kuisimamia
sekta ya uhifadhi nchi wakitoa wito wa kudumisha mahusiano mema baina ya
wananchi na wahifadhi.
0 comments:
Post a Comment