METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, June 21, 2019

WAZIRI BASHUNGWA AWAHAKIKISHIA WAKULIMA WA TUMBAKU MASOKO

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa (kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi wa Mahusiano  kutoka kampuni ya Sigara Tanzania (TCC) Bw. Godson Killiza aliyefika Ofisi ndogo za Wizara Dar es salaam kwa mazungumo.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa (kulia) akiagana na Bw. Godson Killiza Mkurugenzi wa mahusiano wa kampuni ya Sigara Tanzania (TCC) aliyefika Ofisi ndogo za Wizara Dar es salaam kwa mazungumo
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa wa tatu (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi kutoka TCC na Watumishi wa Wizara ya Viwanda na Biashara.

……………..

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa amesema Serikali itatafuta wanunuzi wa zao la Tumbaku endapo Kamapuni iliyokuwa inanunua awali ya TLTC  haitaendelea na ununuzi huo.

Amesema kuwa tayari Kampuni ya GTI imekubali kushirikiana na Serikali kununua zao hilo kutoka kwa wakulima msimu ujao.

Mhe. Bashungwa  ameyasema hayo leo alipokutana na  wawakilishi wa Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC) ambapo aliahidi kufanya mazungumzo  na Waziri wa Kilimo kwa lengo la kujadiliana namna ya kupata kampuni itakayoweza kununua zao la tumbaku kutoka kwa wakulima.

‘’Tutazungumza na kampuni ya awali iliyokuwa ikinunua tumbaku kama watakubali kuendelea kununua zao hilo au kama hawawezi basi serikali itatafuta wanunuzi wengine watakaonunua zao hilo kwa wakulima msimu ujao,’’ alisisitiza.

Aliongeza kuwa wadau wengi wameipongeza serikali kwa kuwa na bajeti rafiki iliyosikiliza wadau wa viwanda na biashara kuhusu masuala ya tozo na kodi mbalimbali.

Bashungwa  alisema Serikali itaendelea kuondoa vikwazo vilivyokuwepo kwenye sekta ya biashara kwa lengo la kuleta unafuu na kukuza biashara, ajira na mazingira rafiki kwa wafanyabiashara wa sekta binafsi.

Naye, Mkurugenzi wa Mahusiano Godson Killiza kutoka TCC alisema kitendo cha serikali kupunguza kodi ya bidhaa mbalimbali ni jambo linaloleta faida kwa wafanyabiashara watanzania kutumia malighafi za ndani kuzalisha bidhaa.

Alisema bajeti ya serikali ya 2019/2020 italeta faida katika ukuaji wa uchumi, kukuza biashara na kupunguza gharama za uzalishaji kwa kampuni nyingi.

Killiza alisema ongezeko la Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa asilimia nane katika biashara yao imesaidia kuongeza ulipaji wa kodi kutoka Sh bilioni 227 mwaka 2017 hadi Sh bilioni 234 mwaka jana.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com