Wito umetolewa kwa wakazi wa Makete
waishio Jijini Dar es Salaam, kuanzisha Kampuni ya Uwekezaji na Mfuko wa
Maendeleo wa Wilaya hiyo utakaoangalia fursa za kiuchumi zinazopatikana
Makete, Mkoani Njombe, ili kukuza pato lao na Taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji
wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Bw. Geoffrey Mwambe, wakati
akifungua Mkutano Mkuu wa Wanachama wa Chama cha Maendeleo Makete (MDA)
uliofanyika Jijini Dar es Salaam.
Bwana Mwambe akasema, fursa ya kuanzisha
kampuni na mfuko utawawezesha wakazi hao kununua hisa na umiliki pamoja
na kuwapa fursa za kutafuta masoko ya bidhaa na huduma zitakazotolewa
ikiwa ni sehemu ya kuitangaza Wilaya hiyo kwa wawekezaji wengine.
“Makete mna fursa nyingi za uwekezaji,
kuna kilimo cha ngano, pareto, viazi, matunda na mbogamboga, pia mnayo
madini mbalimbali, mnao utalii wa ndege na maua kule kwenye hifadhi ya
Kituro, ndugu zangu, uwekezaji katika sekta hizo inawezekana kabisa, pia
mnayo ardhi ya kutosha, ni muhimu muwekeze nyumbani” alisema Mwambe.
Mwambe aliwataka wakazi hao kushirikiana
na kuongeza nguvu katika kutangaza fursa na vivutio vya utalii vilivyopo
katika Wilaya hiyo ambayo imebarikiwa kuwa na hali nzuri ya hewa ya
kuweza kuzalisha mazao mbalimbali ya chakula na biashara.
“Ndugu zangu uwekezaji unawezekana sana
Makete, mna ardhi yenye rutuba,mna hali nzuri ya hewa, umoja wenu ni
bora zaidi kuliko utengano, nawaomba sana muungane na muanzishe Mfuko na
Kampuni ya Wanamakete vitakayokuwa na malengo ya kuiletea maendeleo
Wilaya ya yenu”alisema Mwambe.
Aidha aliongeza Wilaya hiyo inao uwezo
mkubwa wa kuzalisha ngano lakini bidhaa hiyo kwa asilimia kubwa
inaagizwa kutoka nje ya nchi na kuwataka ikutafakari hilo ili kuzalisha
ngano kwa wingi.
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Makete, Bw.
Burton Sinene alisema kwa sasa Wilaya hiyo inahitaji wawekezaji katika
kiwanda cha kutengeneza njiti za meno (bamboo toothpick) kutokana na
kuwepo kwa zao la mianzi, bidhaa ambayo kwa kiwango kikubwa inaagizwa
nje ya nchi kwa ajili ya matumizi ya mezani wakati wa kula.
Katika majadiliano ya kikao hicho wakazi
hao waliiomba Serikali izidi kuimarisha miundombinu ya barabara ili
kuweza kusafirisha mazao toka mashambani kwenda kwenye masoko
mbalimbali, suala ambalo pia litawavutia wawekezaji wengi zaidi.
0 comments:
Post a Comment