METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, June 16, 2019

Tume ya Madini yasisitiza uuzaji wa Madini kwenye Masoko

Afisa Madini mkazi mkoa wa Njombe na Iringa Wilfred Machumu katikati akiambatana na Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula wa kwanza kulia wakiingia kukagua soko la madini ya Dhahabu na Vito mkoa wa Iringa.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula wa kwanza kushoto, Kamishna wa Tume ya Madini Prof. Abdulkarim Mruma wa nne kulia wakiwa kwenye kikao na mwenyeji wao mkuu wa mkoa Ruvuma Christina Mndeme kuhusu ukusanyaji wa maduhuli ya serikali kupitia sekta ya madini.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula mwenye kofia akiwa kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo wa kampuni ya Thomas G. Masuka & Partners kwenye mgodi wa Nyakavangala Isimani mkoani Iringa.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula na Kamishna wa Tume hiyo Prof. Abdulkarim Mruma wakiwa chini kwenye mgodi wa kampuni ya TANCOAL inayo zalisha makaa ya mawe walipotembelea eneo la uzalishaji mgodini hapo.
***********************
Na Issa Mtuwa “WM” Iringa Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula amekemea na kutoa onyo kwa Wachimbaji na wanunuzi wa madini nchini kuacha tabia ya kufanya biashara ya madini nje ya masoko yaliyoteyari na yanayoendelea kuanzishwa mikoa yote hapa nchini.
Prof. Kikula amesema hayo Juni 15, 2019 muda mfupi mara baada ya kukagua soko la madini mkoani Iringa ambako hakuridhishwa na takwimu za uuzaji wa madini ya dhahabu katika soko hilo kuwa spidi ni ndogo akitolea mfano wa takwimu zilizotolewa na Mkaguzi wa Madini kituo cha Iringa Severine Haule kuanzia tarehe 30 Mei, 2019 hadi tarehe 14 Juni, 2019 ni gram 92 tuu za dhahabu zimezalishwa na kupita sokoni hapo.
Amesema serikali haina mzaha kuhusu suala hilo na yeyote atakae kutwa anafanya biashara ya madini nje ya masoko rasmi atakumbana na mkono wa sheria ikiwemo kutaifishwa madini na kila aina ya raslimali iliyotumika kuwezesha ufanyikaji wa biashara hiyo, hivyo ametoa wito kwa wadau wote kujiepusha na utoroshaji wa madini sambamba na kufanya biashara nje ya Masoko.
Ameongeza kuwa, jicho la serikali linaona mbali hivyo asijidanganye mtu. Amesema kuwa ziko taarifa za ujanja ujanja kufanya biashara ya kuuziana madini usiku wilayani Tunduru, wengine kutorosha madini kuelekea Malawi kwa wilaya ya Songea na Mbinga, na Iringa wachimbaji wadogo, wanunuzi wa kati (Brokers) na wanunuzi wakubwa (Dealers) kuuziana madini kwa siri kutofikisha madini kwenye soko. Amesema taarifa zote hizo serikali inazo hivyo amewaomba wadau wote wanaohusika na michezo hiyo waache mara moja na kama wataendelea wajue siku zao si nyingi hivyo wasijitafutie matatizo wakaacha familia zao bila sababu.
Wakati huo huo Mwenyekiti ameendelea kuwasisitiza watumishi wa Tume hiyo mikoa yote nchini kuzingatia uadilifu na kwamba kamwe wasikubali kushawishika kwa rushwa.
Amesema laiti kama yeye angekuwa mwepesi wa kupokea rushwa pengine asingekuwa anaendelea kumsaidia Rais Magufuli kuwatumikia Wananchi kwani yapo majaribu mengi na majaribio ya watu kumpelekea vifurushi na mabegi ya fedha lakini hajawahi kuingia katika mitego hiyo na hajawahi pokea rushwa hata siku moja katika miaka 46 ya maisha yake yote ya utumishi wa umma.
Amewambia watumishi hao kuwa wakae wakijua wale watakao waletea fedha hiyo siri haitabaki kwa mtu mmoja lazima itavuja na huo ndio mwanzo wa kuharibu jina lake hivyo wasikubali rusha ni hatari.
Mwenyekiti Prof. Idris Kikula na Kamishna wa Tume ya Madini Prof. Abdulkarim Mruma wamehitimisha ziara yao katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Njombe na Iringa ambako walikuwa wanakagua shuguli za madini, kuhimiza ulipaji wa maduhuli ya serikali, utatuzi wa migogoro, kusikiliza kero na kutatua, kuongea na wafanyakazi wa tume ya madini, wachimbaji, wafanyabiashara wa madini na kuognea na viongozi wa serikali ngazi ya mikoa na wilaya.
Yaliyojiri kwa ujumla katika ziara hiyo ni pamoja na; kilio cha wachimbaji wadogo katika mikoa mbalimbali kutozwa kodi zaidi na Halmashauri za wilaya na vijiji kinyume cha sheria ya madini, ufinyu wa bajeti, uhaba wa watumishi na vitendea kazi kwa ofisi za tume ya madini mikoani, ucheleweshaji wa utolewaji wa leseni za uchimbaji kwa wachimbaji wadogo, ulipaji wa maduhuli ya serikali, uuzaji wa madini kwenye masoko rasmi, uadilifu na kuepuka rushwa.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com