***************************************************
CHANGAMOTO ya upatikanaji wa
huduma ya maji safi na salama iliyokuwa inawakabili wananchi wa vijiji
vya Nandagala ‘B’ na Ingawali wilayani Ruangwa imekuwa historia baada ya
Ubalozi wa Uturiki kupitia taasisi yake ya Diyanet kuwachimbia visima
virefu.
Visima hivyo viwili vimekabidhiwa
kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa jana (Jumatatu, Juni 3, 2019) na
Muambata wa Ubalozi wa Uturuki anayeshughulikia masuala ya jamii nchini,
Muhammed Cicek. Hafla hiyo imefanyika katika kijiji cha Nandagala ‘B’.
Akizungumza katika hafla hiyo,
Waziri Mkuu amesema Tanzania na Uturuki ni nchi rafiki na kwamba
Serikali ya Uturuki imekuwa ikishirikiana na Serikali ya Tanzania katika
uboreshaji wa huduma za jamii zikiwemo za afya, elimu na maji.
Waziri Mkuu baada ya kuvipokea
visima hivyo amewataka wananchi wa vijiji hivyo kupitia kamati zao za
maji zihakikishe zinaisimamia vizuri miradi hiyo na pia wawe wanatoa
taarifa za mapato na matumizi ya kila mwezi.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu
amemuagiza Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wilaya ya
Ruangwa, Samwel Pyuza ahakikishe huduma ya umeme inafikishwa katika
mradi huo kwa ajili ya kusukuma maji badala ya kutumia jenereta.
Kwa upande wake, Muambata wa
Ubalozi wa Uturuki anayeshughulikia masuala za jamii nchini, Muhammed
Cicek amesema Watanzania na Waturuki ni ndugu, hivyo amefurahi baada ya
wananchi wa vijiji hivyo kupokea zawadi ya visima hivyo
walivyowakabidhi.
Wakizungumza baada ya makabidhiano
hayo, baadhi ya wakazi wa kijiji cha Nandagala ‘B’ wameishukuru
Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa
kuwasogezea huduma ya maji karibu na makazi yao.
Mmoja wa wakazi hao Safina
Angulupele (63) amesema awali kabla ya kisima hicho walikuwa wanapata
maji kutoka katika kijiji kingine na pia hayakuwa na uhakika, hivyo
uwepo wa kisima kwenye kijiji chao ni mkombozi kwao.
Naye mkazi mwingine wa kijiji
hicho Zainab Issa amesema huduma ya maji safi na salama ni muhimu kwa
maendeleo ya jamii, hivyo anaipongeza Serikali kwa kuwafikishia huduma
karibu na makazi. “Sasa hata sisi wazee tunaweza kwenda kisimani na
kuchota maji.”
Serikali ya Awamu ya Tano kupitia
Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo, imedhamiria
kuwafikishia wananchi wote huduma ya maji safi na salama katika umbali
usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.
0 comments:
Post a Comment