Katika kuhakikisha kuwa, wigo wa
matumizi ya Gesi Asilia nchini unaongezeka kwa kufikia wateja wengi, Wizara ya
Nishati kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) wapo katika
majadiliano ya kuhakikisha kuwa Gesi Asilia inasambazwa katika Mikoa mbalimbali
nchini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua leo tarehe 16 Mei, 2019, ameongoza kikao
kati ya Wizara ya Nishati na ujumbe kutoka JICA kilicholenga
kujadili Mpango wa kufikisha Gesi Asilia mikoani kwa wateja mbalimbali wakiwemo
wa majumbani, viwanda, magari, n.k.
Kikao hicho kilichofanyika katika
Ukumbi wa Wizara ya Nishati, Mtumba, jijini
Dodoma kilihudhuriwa na Kaimu Kamishna wa Petroli na Gesi,
Mwanamani Kidaya, Kaimu Mkurugenzi wa Usambazaji Gesi kutoka Shirika la
Maendeleo ya Petroli (TPDC), Mhandisi Emmanuel Gilbert na maofisa
kutoka Idara ya Petroli na Gesi.
Mpango huo unaojadiliwa na Wizara
pamoja na JICA unaangalia namna bora ya kufikisha Gesi Asilia katika mikoa
mbalimbali nchini kwa kuanza na mikoa ya Dodoma, Morogoro, Tanga, Kilimanjaro
na Arusha.
Kikao hicho, kilijadili masuala
mbalimbali ikiwemo njia mbadala za kufikisha Gesi Asilia
katika miji tajwa tofauti na njia iliyozoeleka ya kujenga bomba ambapo njia
zilizoainishwa ni pamoja na kutumia mitungi yenye gesi iliyokandamizwa (
_Compressed Natural Gas - CNG_); na kujenga mitambo midogo ya kubadili gesi
kuwa kimiminika ( _mini - LNGs_) kisha kuisafirisha kwa njia ya barabara
au Reli kwenda mikoa husika.
Baada ya kikao hicho Katibu Mkuu,
aliipongeza JICA kwa kuendelea kushirikiana na Wizara ya Nishati na TPDC katika
kuandaa Mpango huo utakaoleta manufaa kwa nchi.
Aidha, aliiagiza TPDC, kuandaa kikao
cha Wadau ili kujadili Mpango huo na kuukamilisha kabla ya kuanza hatua za
awali za utekelezaji.
CAPTIONS
MOJA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua (katikati)
akiongoza kikao baina ya Wizara ya Nishati, Shirika la Maendeleo la Japan
(JICA) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kilicholenga kujadili
usambazaji Gesi Asilia majumbani.
0 comments:
Post a Comment