Thursday, May 16, 2019

Wizara ya Nishati na JICA wajadili mpango wa kufikisha gesi asilia mikoani



Katika kuhakikisha kuwa, wigo wa matumizi ya Gesi Asilia nchini unaongezeka kwa kufikia wateja wengi, Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) wapo katika majadiliano ya kuhakikisha kuwa Gesi Asilia inasambazwa katika Mikoa mbalimbali nchini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua leo tarehe 16 Mei, 2019, ameongoza kikao kati ya Wizara ya Nishati na ujumbe kutoka JICA  kilicholenga  kujadili Mpango wa kufikisha Gesi Asilia mikoani kwa wateja mbalimbali wakiwemo wa majumbani, viwanda, magari, n.k.

Kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Wizara ya Nishati, Mtumba, jijini Dodoma   kilihudhuriwa na Kaimu Kamishna wa Petroli na Gesi, Mwanamani Kidaya, Kaimu Mkurugenzi wa Usambazaji Gesi kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC),  Mhandisi Emmanuel Gilbert na maofisa kutoka Idara ya Petroli na  Gesi.

Mpango huo unaojadiliwa na Wizara pamoja na JICA unaangalia namna bora ya kufikisha Gesi Asilia katika mikoa mbalimbali nchini kwa kuanza na mikoa ya Dodoma, Morogoro, Tanga, Kilimanjaro na Arusha.

Kikao hicho, kilijadili masuala mbalimbali ikiwemo   njia mbadala za kufikisha Gesi Asilia katika miji tajwa tofauti na njia iliyozoeleka ya kujenga bomba ambapo njia zilizoainishwa ni pamoja na kutumia mitungi yenye gesi iliyokandamizwa ( _Compressed Natural Gas - CNG_); na kujenga mitambo midogo ya kubadili gesi kuwa kimiminika  ( _mini - LNGs_) kisha kuisafirisha kwa njia ya barabara au Reli kwenda mikoa husika.

Baada ya kikao hicho Katibu Mkuu, aliipongeza JICA kwa kuendelea kushirikiana na Wizara ya Nishati na TPDC katika kuandaa Mpango huo utakaoleta manufaa kwa nchi.

Aidha, aliiagiza TPDC, kuandaa kikao cha Wadau ili kujadili Mpango huo na kuukamilisha kabla ya kuanza hatua za awali za utekelezaji.

CAPTIONS

MOJA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua (katikati) akiongoza kikao baina ya Wizara ya Nishati, Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kilicholenga kujadili usambazaji Gesi Asilia majumbani.


No comments:

Post a Comment