Na Munir Shemweta, BUKOBA
Mkutano wa Kuendeleza Mahusiano ya Mpaka wa
Kimataifa kati ya Tanzania na Uganda kwa ajili ya kurahisisha masuala ya
kijamii, Kiuchumi na Kimazingira umemalizika Bukoba mkoani Kagera kwa Katibu
Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt Faraja
Mnyepe na Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Mazingira wa Uganda Alfred Ollot
kusaini makubaliano yaliyofikiwa.
Mkutano huo wa siku mbili ulimalizika juzi na
kuwakutanisha Makatibu Wakuu wa nchi za Tanzania na Uganda kutoka Wizara
zinazoshughulika na masuala ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mambo ya
Nje, Mifugo na Uvuvi, Maji pamoja na Nishati.
Kabla ya mkutano huo, Wataalamu wa sekta
zinazohusika kutoka nchi hizo mbili walikutana na kujadiliana namna bora ya
kukabiliana na changamoto zinazozikabili nchi za Tanzania na Uganda katika eneo
la Mpaka na baadaye kuwasilisha mapendekezo kwa Makatibu Wakuu kwa lengo la
kujadiliwa kwa manufaa ya nchi hizo.
Baadhi ya mambo yaliyojadiliwa kwenye mkutano huo
ni pamoja na Uimarishaji na Uthamini wa Mpaka wa Kimataifa wa Tanzania na
Uganda, Mpango Kabambe wa Utunzaji Mto Kagera na Matumizi Endelevu ya
Rasilimali za Bonde la Mto Kagera kati ya Tanzania na Uganda.
Akizungumza baada ya mkutano huo, Katibu Mkuu wa
Wizara ya Mifugo na Uvuvi Profesa Elisante Ole Gabriel alisema katika siku
mbili za mkutano huo, nchi washiriki zilijadili namna bora ya kuendeleza
mahusiano ya mipakani kwa lengo la kurahisisha mambo ya kiuchumi, kijamii na
kimazingira sambamba na kujadili jinsi ya kuboresha matumizi endelevu ya Rasilimali
za Bonde la Mto Kagera ili ziweze kuleta manufaa kwa nchi za Tanzania na
Uganda.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na
Mazingira wa Uganda Alfred Okidi Ollot alisema, mkutano huo ni njia sahihi ya
kuonesha kuimarika kwa mahusiano ya Tanzania na Uganda na kusisitiza kuwa
kilichofanyika ni kuonesha uhalisia wa ushirikiano kwa lengo la kuwafanya
wananchi wa pande zote kunufaika.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt Faraja Mnyepe alizishukuru pande zote mbili
za nchi za Tanzania na Uganda kwa kufanikisha kufikiwa makubaliano aliyoyaeleza
kuwa yana lengo la kuleta manufaa kwa nchi za Tanzania na Uganda.
0 comments:
Post a Comment