Na Teresia Mhagama, Geita
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, amemwagiza mkandarasi wa ujenzi wa kituo cha kupoza umeme wilayani Geita, kuanza ujenzi wa kituo hicho mwezi wa Sita mwaka huu na kumaliza kazi hiyo mwezi wa Tano mwakani ili kuboresha hali ya umeme mkoani Geita.
Dkt Kalemani aliyasema hayo wakati akiwa kwenye ziara ya kukagua miradi ya umeme inayoendelea kutekelezwa katika Mkoa wa Mwanza na Geita ambapo alikagua kazi ya ujenzi wa kituo cha kupoza umeme wilayani Geita na mradi wa usambazaji umeme vijijini wilayani Sengerema na Chato.
"Msisubiri kusukumwa, jitumeni wenyewe ili mradi huu ukamilike mapema, na wananchi wapate umeme usiokatika mara kwa mara, pia kukamilika kwa kituo hiki kutawezesha mgodi wa dhahabu wa Geita kuunganishwa na umeme wa gridi, kwani sasa wanatumia umeme wa mafuta ambao ni wa gharama kubwa." alisema Dkt Kalemani.
Alisema kuwa, kituo cha kupoza umeme cha Geita ni moja ya kazi zinazotekelezwa kupitia mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kV 220 yenye urefu wa kilometa 55 kutoka Bulyanhulu hadi Geita ambao pia unahusisha upanuzi wa kituo cha kupoza umeme Bulyanhulu, usambazaji umeme katika vijiji 10 vinavyopitiwa na mradi na kubadilisha mita za umeme za kawaida 1500 mkoani Geita.
Aliongeza kuwa, mkandarasi anayejenga kituo cha kupoza umeme cha Geita pamoja na njia ya kusafirisha umeme ni kampuni ya CAMC kutoka China huku mkandarasi atakayesambaza umeme kwenye vijiji vinavyopitiwa na mradi ni kampuni ya STEG na kwamba gharama ya mradi mzima ni Dola za Marekani milioni 23.
Akiwa wilayani Sengerema, Waziri wa Nishati, aliwasha umeme katika Kijiji cha Mnadani na Nyakato na kutoa Siku Saba kwa mkandarasi kampuni ya NIPO kusambaza umeme katika vijiji vyote vya Kata ya Tabaruka.
Dkt Kalemani alisema kuwa, Mkoa wa Mwanza umetengewa jumla ya shilingi bilioni 30 kwa ajili ya mradi wa usambazaji umeme vijijini unaoendelea na unatarajiwa kukamilika Juni mwaka 2020.
Akiwa wilayani Chato, Waziri wa Nishati, aliwasha umeme katika Kijiji cha Mulanda na Maweni ambapo aliwahamasisha wananchi kulipa shilingi 27,000 tu ili waunganishiwe umeme huo utakaowawezesha kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo.
0 comments:
Post a Comment