Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ameahidi kutoa Tsh. Milioni 200
kwa ajili ya ujenzi wa jengo jipya la wagonjwa wa nje (OPD) katika Hospitali ya
Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Waziri Ummy ametoa ahadi hiyo leo wakati alipofanya ziara ya
kutembelea jengo jipya la mama na mtoto (Maternity Block) katika Hospitali hiyo
ili kujionea hali ya utoaji huduma kwa akina mama wajawazito na watoto.
“Ninaahidi kutoa Milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa jengo
jipya la OPD ya kisasa yenye uwezo wa kupokea wagonjwa wengi zaidi tofauti na
OPD iliyopo sasa”. Amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy ameutaka uongozi wa Hospitali hiyo kurekebisha na
kufanya maboresho katika baadhi ya maeneo yaliyoonekana kuwa na changamoto
mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuyapa majina majengo yote ya Hospitali hiyo ili
kuepusha usumbufu kwa wagonjwa pindi wanapotaka kupata huduma katika majengo
tofauti.
Aidha, Waziri Ummy ameutaka uongozi wa Hospitali hiyo kujenga
ghorofa ambayo itakua maalum kwa ajili ya matibabu ya watoto pekee yenye uwezo
wa kulaza watoto wengi sambamba na chumba cha uangalizi maalum kwa watoto
waliozaliwa kabla ya muda (Intensive Neonatal Care Unit) na wale wanaohitaji
uangalizi maalum (ICU).
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Zainab
Chaula amesema Wizara itaendelea kushirikiana na uongozi wa Hospitali hiyo
katika kutatua changamoto mbalimbali zilizoonekana katika Hospitali hiyo ikiwa
ni pamoja kuongeza watumishi wa kada mbalimbali ili kukidhi mahitaji.
“Naomba niwaahidi tutaongeza watumishi wa kada mbalimbali ili
kuziba mapungufu yanayoonekana, lengo likiwa ni kuboresha huduma katika
Hospitali hii inayotegemewa na watu wengi wa Dodoma na kutoka maeneo ya
jirani”. Amesema Dkt. Chaula.
Hata hivyo Dkt. Chaula amewataka watumishi wa Hospitali hiyo
kushirikiana ili waweze kutoa huduma nzuri kwa wagonjwa wanaokwenda hospitalini
hapo.
Katika ziara hiyo iliyoenda sambamba na siku ya Afya Duniani
imejumuisha viongozi mbalimbali wa Wizara akiwemo Mkurugenzi wa Sera na Mipango
Edward Mbaga wameondoka na azimio la kufanya maboresho katika Hospitali hiyo
ikiwa ni pamoja na kujengwa kwa jengo maalum la kupokea wageni mbalimbali
wanaokuja Dodoma.
0 comments:
Post a Comment