METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, September 12, 2016

Viwanda vya TBL Group vyashinda tuzo za uzalishaji bidhaa bora kimataifa

tbi1
Baadhi ya wafanyakazi wa TBL Group wakipokea tuzo kutoka kwa Ma Meneja wa viwanda vya TBL Group walipowasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa JKN wa jijini Dar es Salaam wakitokea nchini Afrika ya Kusini.
tbi2
Baadhi ya wafanyakazi wa TBL Group wakipokea tuzo kutoka kwa Ma Meneja wa viwanda vya TBL Group walipowasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa JKN wa jijini Dar es Salaam wakitokea nchini Afrika ya Kusini.
tbi3
Ma Meneja na baadhi ya wafanyakazi  katika picha ya pamoja kwenye uwanja wa ndege wa Dar wa Salaam
-Bia ya Safari yatangazwa kinara kwa ubora barani Afrika
Kampuni ya TBL Group imezidi kung’ara kimataifa  kutokana na viwanda vyake vya kutengeneza bia vilivyopo kwenye mikoa ya Dar es Salaam,Mbeya,Mwanza na Arusha kushinda tuzo za juu za kimataifa za SABMiller kwa uzalishaji bora ambapo pia bia aina ya Safari Lager imetangazwa kuwa ni bia bora (Champion Beer) barani Afrika.

Kampuni ya SABMiller imekuwa na utaratibu wa kushindanisha viwanda vyake vilivyopo kwenye nchi mbalimbali na kutoa vigezo vya kushindania kigezo kikubwa kimojawapo kikiwa ni ubora wa bidhaa zinazozalishw.

Hafla ya kutangaza viwanda vilivvoshinda na kuvipatia tuzo ijulikanao kama SABMiller Africa Technical Awards ilifanyika jana nchini Afrika na kuhudhuriwa na Maofisa waandamizi wa kampuni hiyo wakiwemo mameneja wa viwanda vya bia kutoka kampuni zake tanzu.

Bia aina ya Safari Lager iliyozalishwa katika viwanda vya TBL vya Dar na Arusha ilitangazwa bia bora barani na kutunukiwa tuzo,kiwanda  cha Dar kikiwa kimeshika nafasi ya kwanza na Arusha nafasi ya pili.

Tuzo nyingine ambazo viwanda vya TBL Group vimeshinda ni tuzo ya uzalishaji wa bia bora ya Castle inayojulikana kama Mick Steward Castle Lager award ambapo kiwanda cha TBL Dar es Salaam kimeshika nafasi ya kwanza,TBL Mbeya nafasi ya pili na TBL Arusha nafasi ya tatu.

Nyingine ni Tuzo ya Upishi Bora wa bia ya mwaka (Brewery of the Year Award),ambapo kiwanda cha TBL Mbeya kimeshika nafasi ya kwanza na kiwanda cha TBL Mwanza kimenyakua nafasi ya pili.Pia kampuni imeshinda tuzo ya kufuata kanuni bora za Ununuzi na Ugavi (Supply Chain and Planning award).

Mkurugenzi wa Ufundi wa TBL Group,Gavin Van Wijk amevipongeza viwanda vyote kwa kuibuka na ushindi wa tuzo kubwa za SABMiller.

“Ushindani ulikuwa mkubwa ukihusisha viwanda vingine kutoka nchi mbalimbali duniani,inafurahisha kuona viwanda vya Tanzania vinachomoza na kushinda tuzo kama hizi,hii inadhihirisha kuwa TBL imejipanga kwenda sambamba na mkakati wa serikali wa kuifanya Tanzania nchi ya viwanda kwa kuwa mafanikio haya yanaletwa na watanzania wenyewe”.Alisema.

Wijk aliwashukuru wateja wote wa bidhaa za TBL Group kwa kuiunga mkono kampuni na aliahidi kuwa kampuni itaendelea kuzalisha bora wakati huo huo ikishiriki kusaidia miradi mbalimbali ya kuboresha maisha ya wananchi hususani katika sekta za kilimo,mazingira,elimu na afya.

Akiongea kwa niaba ya Mameneja wa viwanda vya TBL Group vilivyoshinda tuzo,Meneja wa kiwanda cha Dar es Salaam,Calvin Martin amesema wamefurahishwa kuona viwanda vya Tanzania vinafanya vizuri na kutambuliwa kimataifa “Tuzo hizi zinatokana na mchango wa kila mfanyakazi wa kampuni,tuzidi kuongeza bidii katika kazi tutazidi kufanya vizuri zaidi na tunashukuru wateja wetu wote kwa kutuunga mkono kwa kutumia bidhaa zetu ,tumejipanga kuhakikisha wanazidi kupata bidhaa zetu kwa ubora mkubwa na kwa urahisi popote walipo”.Alisema Calvin.

Wakati huohuo,Mhandisi wa kitanzania,Richmond Raymond ,ambaye alikuwa ni Meneja wa Kiwanda cha TBL cha Mwanza kwa sasa hivi akiwa amehamishiwa nchini Afrika ya kusini kuwa Meneja wa Kiwanda cha  bia cha Polokwane kilichopo nchini Afrika ya Kusini ametunukiwa tuzo maalumu ya kutoa mchango mkubwa kwa kampuni inaojulikana kama SABMiller Brewery Legend  status katika hafla hiyo.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com