Mkurugenzi Mkuu wa taasisi ya Granot Group kutoka nchini Israel Bw Yaron Tamir akimkabidhi Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) taarifa kuhusu kazi wanazozifanya katika nchi mbalimbali duniani, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) akifanya mazungumzo na viongozi wa taasisi ya Granot Group kutoka nchini Israel iliyoongozwa na Bw Yaron Tamir katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Na
Mathias Canal, Dar es salaam
Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omary Mgumba (Mb)
jana tarehe 31 Machi 2019 alikutana na kufanya mazungumzo na wawakilishi wa
Taasisi ya Granot Group kutoka nchini Israel wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa
Taasisi hiyo, Bw Yaron Tamir.
Dhifa hiyo ilifanyika katika Ukumbi wa
Mikutano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambapo
kwa kauli moja wamejadili fursa kwa watanzania kuhusu nafasi za masomo kwa
vitendo kwa wanafunzi waliopo katika vyuo vya kilimo duniani kwa kutumia Mfumo
wa kubadilishana wanafunzi (internship exchange program) kwenda nchini Israel
kujifunza zaidi.
Kwa Tanzania, progamu hiyo ilianza kutekelezwa
katika mwaka wa fedha 2015/16 kwa wanafunzi 20 kutoka Chuo cha SUA kwenda
nchini Israel, mwaka 2016/17 wanafunzi 30 kutoka vyuo vya SUA, Ukiriguru na
Uyole, mwaka 2017/18 wanafunzi 30 kutoka vyuo vya SUA, Ukiriguru, Uyole, Tumbi
na Tengeru.
Kikao hicho kilichohudhuriwa na Mratibu wa
Programu hiyo nchini Tanzania, Dkt. Anna Temu ambae ni mwenyekiti wa Bodi ya
Taasisi ya SUGECO na baadhi ya maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki.
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba ameishukuru
Taasisi hiyo kwa msaada wanaoutoa kwa wanafunzi wa kitanzania waliopo katika
vyuo mbalimbali vya kilimo nchini.
Pia, alisema kuwa, kupitia programu hiyo,
idadi ya wataalamu wa masuala ya kilimo nchini itaongezeka kwa sababu wahitimu
wa masomo hayo wakirudi Tanzania ni lazima ‘wasambaze’ uzoefu na utaalamu
walioupata nchini Israel kwa manufaa yao, wakulima na Taifa kwa ujumla.
Alisema kuwa program hiyo ina umuhimu mkubwa
kwa wananfunzi kutoka nchini Tanzania ili kuhakikisha kilimo kinakuwa chenye
tija na chenye manufaa kwa mkulima hivyo kuongeza kipato cha mkulima,
kutengeneza ajira na pia kuchangia pato la Taifa kwa ujumla.
“Mahusiano baina ya Tanzania na Israel
yamezidi kuimalika kwa manufaa ya nchi hizi mbili na pia, wanafunzi wenye sifa
stahiki watapatikana kupitia uhakiki wa kina utakaofanyika katika vyuo vyao ili
watakaofaulu usaili waweze kwenda nchini Israel kujifunza kwa vitendo zaidi kwa
manufaa yao binafsi, vyuo vyao na Taifa kwa ujumla” Alikaririwa Mhe Mgumba wakati
akifunga Kikao hicho.
Naye, Mkurugenzi wa taasisi hiyo ya Granot
Group kutoka nchini Israel Bw Yaron Tamir alisema kuwa, Taasisi hiyo imekuwa
ikifanya kazi ya kutoa mafunzo kwa wanafunzi waliopo vyuoni kwa kipindi cha
zaidi ya miaka 15 hadi sasa ambapo katika Bara la Afrika programu hiyo
inatekelezwa katika nchi mbalimbali kama vile Ghana, Togo, Burkina Faso, Benin,
Rwanda, Uganda, Ivory Coast n.k.
Tamir alimuhakikishia Naibu Waziri kuwa
wanafunzi hao wakifika nchini Israel wanapewa mafunzo ya nadharia darasani baada
ya hapo wanapelekwa mashambani kujifunza kwa vitendo kwa muda wa siku tano kwa kila
wiki na watakuwa huko kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Mkurugenzi huyo aliongezea kusema kuwa, kilimo
ni biashara, hivyo, wanafunzi wakiwa Israel watajifunza namna ya kulima kwa
tija kwa kuzingatia mbinu bora za kilimo na kutumia zana za kisasa za kilimo na
kujua namna ya kupata masoko ya bidhaa watakazozalisha vile vile, wanafunzi hao
wataweza kufahamu changamoto zilizopo katika Sekta ya kilimo duniani na njia
zinazotumika kuzipunguza.
Dhumuni la safari hiyo ni kuwasaidia vijana
waliopo katika vyuo mbalimbali vya kilimo nchini ili waweze kuwa wakulima
wakubwa wa mazao mbalimbali kama vile, maparachichi, nyanya na hata ufugaji wa
mifugo ya aina mbalimbali kama vile kuku pindi watakapomaliza masomo yao na
hivyo kutengeneza ajira kwa vijana wenzao.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Granot Group
aliongezea kwa kusema kuwa, mwaka huu, wametoa nafasi 100 kwa vijana waliopo
katika vyuo mbalimbali vya kilimo nchini kwenda Israel kujifunza kwa vitendo
kwa kipindi cha mwaka mmoja ikiwa ni sehemu ya masomo ya wanafunzi hao vyuoni
kwao.
Alisema kuwa, vigezo vinavyohitajika kwa
wanafunzi hao kushiriki safari hiyo ni pamoja na: mwombaji kuwa mwanafunzi
katika Chuo cha kilimo, awe raia wa Tanzania anaeweza kuongeza kwa ufasaha
lugha ya kiingereza, mchapakazi, mwajibikaji na mwenye uwezo wa kuishi na watu
wa mataifa mbalimbali duniani.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment