MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC), Salim Asas ameshauri miaka mitano ijayo ya chama hicho iwe ya ‘Siasa na Uchumi,’ kauli mbiu itakayoinua hali kwa wanachama wake kufanya siasa sambamba na kujijenga kiuchumi.
Asas aliyasema hayo wakati akifunga Baraza la Wanawake Tanzania (UWT) la chama hicho Iringa Vijijini lililofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo, mjini Iringa.
“Siasa ndiyo maisha yetu, kwa vyovyote huwezi kukwepa siasa kwenye maisha yako hata kama utaamua kutojihusisha na siasa. Sasa kwa kuwa siasa ni maisha, tuangalie namna bora ya kuwafanya wanachama wetu wawe na hali ya kujiinua kiuchumi,” alisema.
Alishauri uanzishishwaji wa vyama vya ushirika wa kuweka na kukopa akisema vinaweza kusaidia kufufua fursa za kiuchumi kwa jamii na hususani wanawake na hivyo kuwafanya wafaidike na misaada mbalimbali.
“Tanzania ina mipango mbalimbali ya kuwajengea uwezo wa kiuchumi wanawake na makundi mengine ya kijamii ili kuchochea usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana,” alisema.
Katika hatua nyingine, Asas amewapongeza viongozi wa UWT Iringa Vijijini wanaokaribia kumaliza muda wao akisema CCM itawakumbuka kwa kazi kubwa ya kukiimarisha chama hicho waliyoifanya kwa miaka mitano iliyopita.
Kutokana na mchango wao huo, ameahidi kuchangia ujenzi wa nyumba ya Katibu wa UWT wa wilaya hiyo akisema mpango huo unaolenga kuwaondoa watendaji wa chama na jumuiya zake kutoka katika nyumba za kupanga na kuishi katika nyumba za chama nchi nzima.
Ahadi ya Asas ya ujenzi huo iliungwa mkono na Mbunge wa Kalenga Jackson Kiswaga aliyeahidi kutoa mchango wa awali wa Sh Milioni moja huku akiwahakikishia wanawake hao kwamba atachanga zaidi.
Katika taarifa yake ya utekelezaji Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Bi Lena Hongole ametaja mafanikio yaliyopatikana kuwa ni kuundwa kwa Vikundi 1500 kutoka vikundi 82 vya awali, ambapo pia vikundi 80 vinapata mkopo. Pia ametaja kuanzishwa kwa viwanda 68 vinavyomilikiwa na wanawake sambamba na kufufua shamba la jumuiya na viwanja vitatu vimenunuliwa kwa ajili ya uwekezaji.
Changamoto iliyotajwa katika taarifa hiyo ni ukosefu wa mabweni kwa wasichana mbunge wa jimbo hilo Mhe. Jackson Kiswaga amesema utekelezaji wa ujenzi wa mabweni kwenye jimbo hilo unaendelea.
Kuhusu mikopo kwa wanawake mbunge anasema miongoni mwa sifa za wanawake wanaostahili kupatiwa mikopo kupitia mfuko wa jimbo ni vikundi vya maendeleo visivyo vya kisiasa
Katika kipindi hiki ambacho chama hicho kinaendelea na uchaguzi wake wa ndani wa ngazi mbalimbali, Asas alitoa mwito kwa wana CCM kuwaogopa wajasiriamali hao kama ukoma ili kukinusuru kisipate viongozi wa ovyo, wasio na uwezo na dhamira ya dhati ya kukitumikia kwa kujitolea.
“Tuwe waangalifu sana katika uchaguzi huu, tusichague viongozi kwa Sh 5,000 au Sh 10,000. Tujiepushe na aina yoyote ya rushwa katika uchaguzi huu, vinginevyo tutapata viongozi watakaotugharimu kwa miaka mitano ijayo,” alisema.
0 comments:
Post a Comment