Kwa
mara ya kwanza Barani Afrika, Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kufanya mafunzo
ya kuwajengea uwezo wadau wa Afya moja juu ya namna ya kufanya tathmini ya vimelea hatarishi vya
magonjwa kwa kutumia dhana ya Afya moja. Mafunzo hayo yamewakutanisha wataalam
na wadau wa Afya moja kutoka sekta mbalimbali, hususan sekta za afya ya
binadamu, wanyama, kilimo na mazingira.
Kufuatia nchi ya Tanzania kuwa imepiga hatua katika uratibu
wa masuala ya Afya moja,
ambayo ni dhana inayojumuisha sekta ya afya ya binadamu, wanyamapori, mifugo
na mazingira katika kujiandaa, kufuatilia na kukabili magonjwa
yanayoathiri binadamu, hali hiyo imechagiza kuchaguliwa kuwa nchi ya kwanza
barani Afrika kwa wataalam wa sekta za
Afya hapa nchini kupewa mafunzo hayo.
Mafunzo
hayo yaliyofanyika kuanzia tarehe 25-28 Machi, 2019, Jijini Dar es salaam,
yaliendeshwa na wataalamu kutoka Makao makuu ya
Shirika la Afya Duniani (WHO), Makao makuu ya Shirika la Chakula Duniani
(FAO), pamoja na Shirika linaloshughuliks na Afya ya Wanyama (IOE). Wataalamu
hao wameweza kuwapa mafunzo wataalamu wa sekta za Afya hapa nchini juu ya namna
ya kufanya tathmini hiyo kwa magonjwa ya Kichaa cha mbwa, Kimeta na Homa ya
Mafua ya ndege.
Akiongea
wakati wa kufungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri
Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe, alibainisha kuwa ushirikiano wa wataalam na sekta
za Afya kwa kutumia dhana ya Afya Moja
hivi sasa ni agenda ya dunia nzima. Aidha amefafanua kuwa dhana hiyo inapunguza gharama katika
kushughulikia tishio la magonjwa
yanayotokana na vimelea vyenye uwezo wa kutoka kwa wanyama na kwenda kwa
binadamu na hata mimea (mazingira) na kusababisha magonjwa na hata usugu wa
vimelea vya magonjwa.
Wakiongea
kwa nyakati tofauti washiriki wa mafunzo
hayo wamebainisha kuwa wamekuwa
wakifanya tathmini za vimelela hatarishi vya magonjwa hapa nchini lakini
tathmini hizo zimekuwa ni za kisekta kwani hazikuwa zinazingatia ushirikiano
kwa maana ya dhana ya Afya moja. Aidha walifafanua kuwa mafunzo hayo
yamewawezesha kuandaa nyenzo ya kitaifa ya kufanya Tathimini kwa Dhana ya Afya
Moja ambayo itawaongoza Wataalamu
hususani wanapokuwa katika maeneo halisi yanakotokea magonjwa.
Aidha,
washiriki hao walieleza kuwa Dhana ya
Afya Moja inatumika zaidi kwa kuzingatia kuwa vimelea vingi vinavyo sabababisha
magonjwa kwa binadamu asilimia (60%) vinatoka
kwa wanyama pori na mifugo na maambukizi yanatokea pale binadamu anapoingilia
maskani ya wanyama hao bila tahadhari. Hata hivyo, kwa nchi za Afrika hali ni
hatarishi zaidi kwa kuzingatia kuwa Bara la Afrika hususan sehemu zinazokaribia
mapori makubwa ya wanyama (Congo Basin) ni kitovu cha magonjwa ya mlipuko kama
vile Ebola, Homa ya Bonde la Ufa(RVF), Marburg na mengineyo.
Walibainisha kuwa, Kupitia matokeo ya
mwingiliano kati ya wanyama na binadamu, wadau wa afya moja wanawajibika
kupanga mikakati mbalimbali ya udhibiti, ulinzi na usalama katika kuzuia,
kujiandaa na kukabali magonjwa ambukizi. Moja ya mkakati ulioibuliwa Kitaifa na
kimataifa ni kujiandaa kwa kuwafundisha
wataalam wa sekta mbalimbali za
afya jinsi ya kufanya tathmini ya
hatari ya vimelea vya magonjwa ambukizi kwa ushirikiano.
Tarehe 13
Februari 2018, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim
Majaliwa alizindua Dawati la Uratibu la Afya moja chini ya Ofisi ya Waziri
Mkuu, likiwa na lengo la kusimamia na kuratibu shughui za Afya moja nchini. Kwa kutambua umuhimu huo Idara ya Uratibu Maafa
Ofisi ya Waziri Mkuu, kupitia Dawati la Uratibu wa Afya moja kwa
kushirikiana na WHO, FAO, IOE na
wadau wengine wa Afya moja waliandaa na kuratibu mafuzo hayo.
0 comments:
Post a Comment