LICHA ya kwamba mengi
yameandikwa kuhusu kiwanja cha ndege cha Songea kilichopo Ruhuwiko Manispaa ya
Songea mkoani Ruvuma,bado kuna mengi yanayokihusu kiwanja hiki.
Historia inaonesha
kuwa kiwanja cha ndege cha Songea kilianzishwa mwaka 1950 ambacho kilikuwa
kinamilikiwa na mtu binafsi aliyefahamika kwa jina moja la Robert.
Meneja wa Kiwanda cha
Ndege Songea Jordan Mchami anasema ilipofika mwaka 1963 serikali ilichukua
umiliki wa ,kiwanja hicho kutoka kwa mtu binafsi na kuanza kukiendesha kiwanja
hicho.
Hata hivyo anasema
wakati serikali inakichukua kiwanja hicho,barabara ya ndege ilikuwa ni ya vumbi
na kwamba ilipofika mwaka 1979,serikali iliona umuhimu wa kukikarabati kiwanja
hicho kwa kukiwekea lami.
“Wakati serikali
inakarabati kiwanja hicho kwa kukiwekea lami ,barabara ya ndege ilikuwa na
urefu wa meta 1625 na upana wa meta 30,uwanja uliendelea kutumika kwa kutumia
ndege ndogo zenye uwezo wa kubeba abiria 13’’,anasema Mchami.
Kwa mujibu wa Meneja
huyo,ilipofika mwaka 2017,barabara ya ndege katika kiwanja cha Songea ilikuwa
imechakaa sana hivyo serikali iliona umuhimu wa kukarabati kiwanja hicho kwa
kuongeza urefu wa barabara ya kuruka na kutua ndege toka urefu wa awali wa meta
1625 kwa upana wa meta 30 na kufikia meta 1740 ambapo upana wake ulibakia meta
30.
Kwa upande wake
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Lasack Alinanuswe anasema ukarabati
wa kiwanja hicho. umetekelezwa na kampuni ya CHICCO kutoka nchi ya Jamhuri ya
China na kusimamiwa na Wakala wa Barabara TANROADS kwa gharama ya shilingi
bilioni 37.
Anazitaja kazi ambazo
zimehusika kwenye ukarabati na upanuzi
wa kiwanja hicho kuwa ni urefushaji wa barabara ya kutua na kuruka ndege kutoka
meta 1625 hadi meta 1740.
Hata hivyo
anabainisha kuwa mwisho wa pande zote za
kutua ndege kuna eneo la usalama(Stop way) lenye urefu wa meta 60 kila upande
hivyo kufanya barabara yote kuwa na urefu wa meta 1860
Kulingana na Meneja
huyo wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma,maeneo mengine yaliyokarabatiwa ni eneo la maegesho madogo ya ndege yenye ukubwa
wa meta 70 kwa meta 40 na kwamba matumizi ya maegesho hiyo ndogo ya ndege ni
kuegesha ndege za dharura na ndege za kijeshi.
Mhandisi Alinanuswe
anasema katika kiwanja hicho kumejengwa maegesho kubwa ya ndege yenye uwezo wa
kuegesha ndege sita kubwa aina ya bombardier kwa wakati mmoja yenye urefu wa
meta 139 na upana wa meta 126.
Hata hivyo anasema
maegesho ya ndege ya zamani ilikuwa ni
ndogo yenye urefu wa meta 72 kwa meta 55 na kwamba katika ukarabati
huo,limejengwa jengo jipya kwa ajili ya abiria lenye uwezo wa kuchukua abiria
kati ya 150 hadi 200 ambapo jengo la zamani la abiria lilikuwa na uwezo wa
kuhifadhi abiria 75 tu.
Meneja Kiwanja cha
Ndege Songea,anazitaja fursa zilizopo katika kiwanja hicho kuwa ni maeneo ya kupangisha wawekezaji kwa ajili ya
kuweka maduka,hoteli pia kuna maeneo ambayo kiwanja cha ndege Songea kinaweza
kuingia ubia kwa kutoa ardhi na wawekezaji kujenga na baada ya kumaliza mkataba
eneo linabaki kuwa mali ya kiwanja cha ndege.
Anaitaja fursa
nyingine inayopatikana kwenye kiwanja hicho,ni fursa ya biashara ya taksi kwa
ajili ya kusafirisha abiria toka katika kiwanja cha ndege hadi mjini Songea.
Akizungumzia mwenendo
wa abiria tangu kurejeshwa kwa safari za abiria za ndege za ATCL Feburiari 17
mwaka huu,Meneja Kiwanja cha Ndege Songea anasema mwitikio wa abiria ni mzuri
kwa sababu ndege iliyokuwa inatoa huduma kabla ya ATCL ilikuwa ni ndogo yenye
uwezo wa kubeba abiria 13 tu na nauli yake kwenda pekee ilikuwa ni zaidi ya shilingi
500,000.
“Hivi sasa kupitia
ndege ya serikali za ATCL yenye uwezo wa kubeba abiria 76,nauli kwenda tu ni
shilingi 250,00,kwenda na kurudi ni shilingi 370,000 kwa hiyo abiria
wamepunguziwa mzigo wa nauli’’,anasema Mchami.
Anasisitiza kuwa
kutokana na hali hiyo siku hadi siku idadi ya abiria inaendelea kuongezeka
ambapo hivi sasa ratiba ya ndege ni mara mbili kwa wiki,siku za Jumatano na
Jumapili ambapo uzoefu unaonesha kuwa siku ya Jumapili kunakuwa na idadi kubwa
ya abiria.
“Tunatarajia
kuwasiliana na ATCL Makao makuu kuona uwezekano
wa kubadilisha ratiba ya ndege ikiwezekana iwe siku za Jumatatu,Jumatano
na Ijumaa ili Ijumaa jioni watu wanaweza
kutoka kazini kuamua kusafiri na Jumatatu Asubuhi kurejea kazini Songea, kwa
kifupi idadi ya abiria inaridhisha’’,anasisitiza Mchami.
Mkuu wa Mkoa wa
Ruvuma Christina Mndeme anasema kiwanja cha ndege wa Songea ni rasilimali adimu inayoweza
kusaidia kukuza uchumi wa mji wa Songea na Mkoa mzima wa Ruvuma hasa kukuza
sekta ya utalii,baada ya kuanzishwa mpango mkakati wa kukuza utalii katika mkoa
wa Ruvuma.
0 comments:
Post a Comment