Na Stella Kalinga, Simiyu
Katibu MTENDAJI wa Baraza la Taifa la
Mitihani nchini (NECTA) amewataka wanafunzi wa kidato cha sita nchini
wanaotarajia kufanya mtihani wao wa mwisho mapema mwezi Mei, 2019 kuepuka aina
yoyote ya udanganyifu kwenye mtihani huo.
Dkt. Msonde ameyasema hayo wakati
akiongea na wanafunzi wa kidato cha sita mkoani Simiyu waliopo kwenye kambi ya
kitaaluma katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa, ambayo inayohusisha
wanafunzi 1166 kutoka shule 12 zikiwemo 10 za umma na mbili za binafsi zenye
kidato cha sita.
"Niwatake msifanye asilani
habari yoyote ya udanganyifu kwenye mtihani wenu, mkifanya hayo tu kwanza
yatawafanya mshindwe lakini pili tutakaponusa tu harufu yoyote ya udanganyifu
tutawafutia matokeo"alisema Dkt. Msonde.
Wakati huo huo Dot. msonde amewataka
wanafunzi hao kuondokana na dhana kwamba mtihani wa Taifa ni mgumu hali
inayopelekea kuwa na homa ya mtihani(hofu), badala yake wajiamini na wajiandae
vema kwa kuzingatia waliyofundishwa na walimu wao.
Pamoja na hayo amewapongeza viongozi
wa mkoa wa Simiyu kwa ubunifu wao wa kuanzisha kambi za kitaaluma hatua
inayopelekea mkoa huo kupiga hatua ya katika ufaulu wa mitihani ya kidato cha
sita na kidato cha nne.
Awali akimkaribisha Katibu Mtendaji
wa NECTA, Afisa Elimu mkoa wa Simiyu, Mwl. Ernest Hinju amesema kuwa
awali mkoa ulikuwa na ufaulu mbaya lakini kupitia kambi ufaulu umepanda kuanzia
matokeo ya kidato cha sita kutoka nafasi ya 26 mwaka 2017 hadi nafasi ya 10
mwaka 2018 na kidato cha nne kutoka nafasi ya 12 mwaka 2017 hadi nafasi ya 9
mwaka 2018.
Akiongea kwa niaba ya walimu mkuu wa
shule ya sekondari ya wasichana Maswa Mwl. Kuyunga Jackson amesema kuwa vijana
wa kidato cha sita Simiyu wamepikwa vizuri kitaaluma hivyo matarajio yao ni
kuingia tatu bora kitaifa.
Katika hatua nyingine wanafunzi
waliopo kambini hapo wamesema kuwa ujio wa katibu mtendaji NECTA umekuwa chachu
ya ufaulu wao na kuahidi kuyafanyia kazi yale yote aliyoyaeleza ikiwemo kuepuka
udanganyifu pamoja na kuondoa homa ya mtihani.
"Tunakushukuru Sana kwa ujio
wako umetujenga na kutuondolea hofu ya mtihani, tutafanyia kazi uliyotueleza,
tunakuhakikishia hatutajihusisha na udanganyifu wowote kwa sababu walimu
wametuandaa vizuri na tunajua udanganyifu unaweza kusababisha tusifikie
ndoto zetu; tutazingatia yote tuliyofundishwa na walimu wetu" alisema
Julieth John.
0 comments:
Post a Comment