METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, June 28, 2018

MD ILEMELA: JAZENI TAARIFA SAHIHI ZA WALENGWA WA TASAF




Watumishi wa huduma za afya wametakiwa kujaza taarifa sahihi za walengwa wanaonufaika na mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF ili kuepuka tafsiri tofauti za taarifa zinazotolewa na vituo vya afya.

Kauli hiyo imetolewa leo na mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela ndugu John Wanga wakati akifungua kikao kazi cha  siku moja kwa watoa huduma za afya kutoka vituo vyote vya afya vinavyohudumia walengwa hao ndani ya manispaa yake ambapo amewaasa kuhakikisha wanajaza taarifa sahihi za walengwa hao pindi wanapofata huduma katika vituo vyao sambamba na kuelekeza juu ya kuwepo watumishi maalumu watakaohusika na upitiaji wa fomu za walengwa hao ili kuongeza ufanisi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma.

‘… Wanapokuja walengwa wa mpango wa kunusuru kaya masikini kufata huduma katika vituo vyenu vya afya nawaomba sana mjaze taarifa sahihi sio mnajijazia tu bora liende  pia mtambue mnapojaza taarifa zisizo sahihi zinapokwenda kutafsiriwa lazima zitaleta picha tofauti …’ Alisema

Aidha mkurugenzi huyo ameongeza kuwa hata vumilia mtumishi yeyote atakaekwenda kinyume na maelekezo hayo na hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa kwa mtumishi yeyote ataebainika kutoa taarifa zisizosahihi na asijefuata utaratibu.

Kwa upande wake mratibu wa TASAF manispaa ya Ilemela ndugu Frank Ngitaoh mbali na kubainisha mafanikio yaliyopatikana kupitia mpango huo ikiwemo kukwamua walengwa zaidi ya 2509 katika umasikini kwa kuwapa mtaji ili kuanzisha miradi midogo midogo  ya kukuza kipato amebainisha juu ya mkakati endelevu walionao utakaosaidia walengwa hao kujikwamua kiuchumi hata baada ya kuisha kwa mpango huo kwa kuwaunganisha walengwa kupitia vikundi ili kushiriki shughuli za kujiongezea kipato.

Nae mwakilishi wa mganga mkuu wa wilaya hiyo ambae pia ni mratibu wa mpango wa huduma za afya ya jamii iliyoboreshwa  (CHF) Bi Gisela Orasa mbali na kushukuru kwa kufanyika kikao kazi hicho amewataka wahudumu wa afya na wawezeshaji wa mpango wa kunusuru kaya masikini kushirikiana kwa pamoja katika kuwaelimisha walengwa wa mpango huo kujiunga katika mfuko huo wa huduma za afya ili waweze kujihakikishia upatikanaji wa huduma bora za afya huku akitoa rai kwa wahudumu wenzake juu ya kuzingatia weredi na taaluma yao katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Akihitimisha kikao kazi hicho afisa ufuatiliaji wa mpango huo ndugu Kagwe Samson amewataka wahudumu hao wa afya kuwa wakarimu pindi wanapowahudumia walengwa wa mpango wa kunusuru kaya masikini ili kuondoa unyanyapaa sanjari na kwenda sambamba na malengo ya serikali chini ya mheshimiwa Rais Daktari John Magufuli ya kupambana na umasikini unaolikabili kundi kubwa la watu katika jamii.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com