Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangala akisisitiza jambo wakati akizungumza na Watumishi wa Wizara hiyo kuhusu umuhimu wa kutekeleza maagizo kwa wakati yanayotolewa na Viongozi wa Wizara hiyo katika kikao cha Baraza la 26 la Wafanyakazi wa Wizara hiyo kilichofanyika leo Jijini Mwanza.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla, Naibu Waziri wa Wizara, Mhe, Constantine Kanyasu wakiwa wameshikana na watumishi wengine hukuwakiimba wimbo wa mshikamano Daima katika Kikao cha Baraza la 26 la Wafanyakazi kilichofanyika leo jijini Mwanza.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi
Kigwangala amewataka Watanzania kuondokana na dhana iliyojengeka miongoni mwao
kuwa watumishi wa Wizara hiyo hususan wahifadhi wa wanyamapori na
Misitu ni watu katili wanaowatesa Wananchi.
Kauli hiyo ameitoa leo wakati akifungua mkutano wa
26 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo uliofanyika katika Chuo cha Taaluma
ya Wanyamapori Pasiansi jijini Mwanza.
Amesema watumishi hao ni watu wenye utu na weledi
wa hali ya juu na wanaozingatia sheria katika kutimiza majukumu yao na
hulazimika kutumia nguvu wakati wakipambana na majangili wanaokutwa katika
maeneo ya hifadhi wakifanya vitendo vya ujangili.
‘’ Ulinzi wa Rasilimali za nchi ni jukumu letu
sote, wizara imepewa dhamana ya kusimamia na kuongoza kwa niaba ya watanzania,
kama kuna watumishi wa Wizara hii wanaowanyanyasa wananchi naomba walete
ushahidi kwetu ili tuwachukulie hatua’’ amesema Dkt. Kigwangala.
Waziri Kigwangala amesikitishwa na idadi ya
watumishi walipoteza maisha kwa ajali na wengine kuuwawa na majangili wakati
wakipambana nao katika maeneo yote ya hifadhi nchini na kutoa wito kwa
wananchi wote wenye taarifa au ushahidi juu ya vitendo vyovyote vya kihalifu
kuziwasilisha katika mamlaka zinazohusika.
Amesema kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua
wale wote wanaojihusisha na vitendo vya ujangili na uhalifu katika maeneo ya
hifadhi na wale wote wanaoshirikiana na makundi ya watu wenye nia ovu ya
kukwamisha juhudi za uhifadhi wa rasilimali za Taifa.
Ametoa wito kwa wananchi kuheshimu sheria za
uhifadhi na kuepuka kuvamia maeneo ya hifadhi kwa shughuli za kijamii na
ufugaji akitoa wito kwa viongozi mbalimbali wa Siasa kuunga mkono juhudi za
wizara za ulinzi wa maeneo ya hifadhi kwa kuwaelimisha wananchi wanaowaongoza
kujiepusha na vitendo vya uvamizi wa maeneo ya hifadhi badala ya kuwatetea.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili
na Utalii, Prof.Adolf Mkenda akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho
amesema kuwa jumla ya watumishi 23 walifariki dunia wakati wakitekeleza
majukumu ya uhifadhi na 5 walijeruhiwa na majangili
wakiwa kazini.
Prof. Mkenda amesema kuwa waliofanya vitendo
hivyo hawaitakii mema Tanzania na ni maadui wa shughuli za uhifadhi
nchini akiongeza kuwa Serikali itaendelea kusimama na kuwatetea watumishi na
askari wa wanyamapori wanaotimiza majukumu yao kwa kuzingatia sheria.
0 comments:
Post a Comment