Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe.Omary Mgumba akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu katika Mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Bukingwaminzi Kata ya Zagayu wakati wa ziara yake wilayani humo Machi 06, 2019.
Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe.Omary Mgumba(kushoto) akiteta jambo na Mbunge wa Itilima Mhe. Njalu Silanga wakati wa Mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Bukingwaminzi Kata ya Zagayu wakati wa ziara yake wilayani humo Machi 06, 2019.
Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe. Benson Kilangi akiwasilisha taarifa ya wilaya kwa Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe.Omary Mgumba wakati alipotembelea wilaya hiyo Machi 06, 2019
Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omary Mgumba ametoa
wito kwa wakulima Mkoani Simiyu kuondokana na dhana potofu kuwa matumizi ya
mbolea yanazeesha ardhi badala yake wazingatie matumizi sahihi ya mbolea
katika kilimo ili kuongeza mavuno, tija na uzalishaji katika kilimo.
Mhe. Mgumba ameyasema hayo Machi 06, 2019 wakati akizungumza
na wananchi wilayani Itilima Mkoani Simiyu, katika Mkutano wa hadhara
uliofanyika katika Kijiji cha Bukingwaminzi kata ya Zagayu wilayani humo wakati
wa ziara yake ya kikazi mkoani Simiyu.
Ameongeza kuwa siyo kweli kwamba matumizi ya mbolea
yanazeesha ardhi badala yake mbolea inasaidia kutibu ardhi na kupelekea
wakulima kuongeza mavuno na tija katika uzalishaji wa mazao na kuwawezesha
kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
“Nimeambiwa
hamtaki kutumia mbolea kwa madai kwamba mkitumia mbolea inazeesha ardhi siyo
kweli, mbolea hizi haziharibu ardhi yetu bali zinakwenda kutibu ardhi;ndiyo
maana watu wa Ruvuma, Njombe, Iringa, Mbeya , Songwe, Rukwa na Katavi
wanaongoza kwa kuzalisha mahindi nchini wenzetu ni wajanja wanatumia Mbolea”alisema
Akizungumzia
suala la viuatilifu Mgumba amewahakikishia wakulima wa zao la pamba mkoani
Simiyu kuwa tayari bodi ya pamba imeshatoa chupa 1000 za viuatilifu/viuadudu
ambapo kila wilaya itapata chupa 200.
Katika hatua
nyingine Mhe. Naibu Waziri amezungumzia suala la bei ya pamba ambapo amesema
Serikali inaendelea kuandaa mazingira wezeshi kwa wanunuzi wa pamba wa ndani na
nje ya nchi kununua pamba ya wakulima kwa bei nzuri na kubainisha kuwa
utaratibu utakaotumika ni wa soko huria.
Kwa upande
wake Mbunge wa Jimbo la Itilima, Mhe. Njalu Silanga pamoja na kuomba pamba
iuzwe kwa bei ya soko huria na kuongezewa viuatilifu, ameomba maghala ya
kuhifadhia pamba yajengwe kupitia sehemu ya fedha inayotolewa na wakulima
katika Vyama vyao vya Ushirika ili pamba ihifadhiwe vizuri na tija ionekane.
Naye Mkuu wa
Wilaya ya Itilima, Mhe. Benson Kilangi amesema jitihada zinaendelea kufanyika
kuwahamasha wakulima wote wa pamba kujiunga na vyama vya ushirika ambapo
amesema hadi sasa ni wakulima 11,700 kati ya 38,910 wako katika
vyama vya ushirika vipavyo 56.
Nao baadhi ya
wananchi waliopata nafasi ya kuwasilisha maombi na kero zao kwa Naibu Waziri wa
Kilimo wameomba viuatilifu/viuadudu vilivyotolewa na bodi ya pamba viwafikie
wakulima kwa wakati.
Naibu Waziri Mgumba yuko mkoani Simiyu katika ziara
ya kikazi yenye lengo la kukagua shughuli za kilimo na ushirika zinavyoendelea
na kukagua shughuli za miradi ya umwagiliaji akiwa Wilayani Itilima amepata
nafasi ya kuzugumza na wananchi kupitia mkutano wa hadhara.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment