Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo
amewaagiza wakuu wa Wilaya za Mkoani Rukwa kuhakikisha wanakuwa na utaratibu wa
pamoja katika kutembeleana na kuelezana changamoto na mafanikio katika maeneo
ya mradi wa ujenzi wa hospitali za wilaya ili kujenga hospitali hizo katika
hadhi sawa na hatimae kupeana ujuzi wa utekelezaji wa mradi huo.
Amepongeza ushirikiano unaoonyeshwa na uongozi wa
wilaya ya Nkasi unaoongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo mh. Said Mtanda pamoja na
wabunge, madiwani na mkurugenzi na kusifu mafunzo waliyoyapata na kuyarekebisha
wakati wa utekelezaji wa ujenzi wa vituo vitatu vya afya katika wilaya hiyo na
kuonyesha dalili za kutojirudia kwa makosa waliyoyafanya wakati wakitekeleza
ujenzi wa vituo hivyo.
“Wakuu wa Wilaya waweke program ya kutembeleana kwa
pamoja ili kujifunza, wanakuja kwa mfano (wilaya ya) Nkasi, wanakwenda wilaya
ya Sumbawanga, Wanakwenda wilaya ya Kalambo halafu watakaa chini wafanye
tafakari ili waone ni namna gani wanweza wakasimamia vizuri hizo hospitali zetu
za wilaya kwasababu tunapaswa tuwe na kitu bora, hospitali zote tatu ziwe bora
ndani ya mkoa wetu,” Alisisitiza.
Alisema kuwa halitakuwa jambo jema kwa wilaya moja
kuwa na ufanisi sana ilihali wilaya nyingine inakuwa na changamoto na hivyo
vyema wakaungana kama timu na kutembelea miradi hiyo ya ujenzi wa hospitali za
wilaya ili kila mmoja aweze kujifunza kutoka kwa mwenzie.
Ameyasema hayo baada ya ziara yake ya kutembelea
ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Nkasi pamoja na ujenzi wa hospitali ya Wilaya
ya Sumbawanga ili kujionea changamoto mbalimbali zinazoukabili mradi huo ambao
unatakiwa kuisha mwishoni mwa mwezi wa sita mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment