Mkuu wa Mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo
amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa ACP Mathias Nyangi kuhakikisha
anafanya msako wa waganga wa kienyeji katika mkoa na kuwakamata wale wote
wanaofanya uganga wa kienyeji bila ya kuwa na leseni halali za kuwaruhusu
kufanya shughuli hizo.
Ametoa agizo hilo baada ya kusikiliza vilio
vya wananchi wakati wa mkutano ulifanyika mtaa wa Vuta, Kata ya Kizwite, mjini
Sumbawanga, wananchi waliokuwa wakiomboleza vifo vya watoto wawili na mmoja
kubaki mahututi katika hospitali ya rufaa ya mkoa baada ya mganga wa kienyeji
kuwateka na kuwaficha katika gari lake chakavu tangu watoto hao kupotea tarehe
21.3.2019 na wawili kupatikana wakiwa wamefariki tarehe 23.3.2019 baada ya
mmoja aliyepona kutoroka na kuwajulisha wananchi kilichotokea.
Amesema kuwa msako huo wa waganga wa kienyeji
ufanyike katika wilaya zote tatu za mkoa ili kuwahakikishia wananchi amani na
utulivu ambayo imekuwepo kwa miaka yote na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano
katika kuhakikisha wanawafagia waganga hao wanaonyesha dalili za kuvuruga
utulivu uliopo katika mkoa.
“RPC fanya Operesheni kali ya waganga wa
Kienyeji ndani ya Mkoa huu, wale ambao wana leseni tutajua hukohuko kwamba huyu
ana leseni n ani halai au siyo halali na kama sio halali basi huyo ni halali
yako, na kama kuna mganga wa kienyeji asiye na leseni, huyo ndio kabisa halali
yako zaidi, kuanzia sasa hivi bonde la ziwa Rukwa kule Nkasi, Kalambo,
Sumbawanga yenyewe hapa kote, opresheni ipite ya kamatakamata waganga wa
kienyeji, tumechoka,” Alisisitiza.
Wakati wakitoa malalamiko yao kwa mkuu huyo
wa mkoa, wananchi hao walisema kuwa vifo vya watoto hao vinahusishwa na Imani
za kishirikina ambapo kumekuwa na wimbi la vijana wanaoonekana wakila, wakinywa
na kuvaa vizuri bila ya kujulikana shughuli zao maalum wanazofanya jambo mbalo
limekuwa likiwaumiza kichwa wananchi hao na kukosa majibu.
Mmoja wa wananchi hao Debora Maenge alisema “
Nasikitika kwa tukio hili lililotokea mtaa wa Vuta, huyu mtu tunaishi nae
jirani sana, tunajua ni mtu mwema, kumbe ni mtu ambae sio mwema na hafai kabisa
katika jamii, cha kushanga alikuwa na vibali ambavyo alikuwa akijitambulisha
kuwa yeye ni mganga wa jadi, vibali hivi vinatolewa serikalini, Je serikali
yetu mtaendelea kutoa vibali hivi ili watu waendelee kuuawa kiasi hiki?
serikali angalieni mnapotoa vibali je ni waganga Kweli?” Aliuliza.
Mh. Wangabo alitembelea eneo la nyumba ya
mganga huyo wa kienyeji ambayo gari alilowafichia watoto ilikuwamo na kukuta
nyumba hiyo ikiwa imevunjwa na gari la mganga huyo kuchomwa moto na wananchi
wenye hasira kali.
Watuhumiwa James Kapyela (52) pamoja na mtoto
wake Michael Martin (14) wa tukio hilo la mauaji ya watoto Nicolous Mwambage
(7) pamoja na Emanuel Juma (4) hivi sasa wanashikiliwa na polisi huku uchunguzi
wa awali ukionyesha watoto hao walifariki kwa kukosa hewa baada ya kufungiwa
ndani ya gari chakavu aina ya Chaser Saloon iliyokuwa haitumiki na vioo vya
gari hiyo kufungwa.
Maelezo ya Picha.
IMG_7579 - Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo akitoa pole kwa wazazi waliofiwa na watoto wao alipotembelea hospitali
ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa mara tu baada ya kupata taarifa ya vifo vya watoto
wawili na mmoja kuwa mahututi baada ya kupatikana tangu kupotea kwao tarehe
21.3.2019.
IMG_7585 - Eneo la Nyumba ya mtuhumiwa ambaye
ni Mganga wa Kienyeji wa mtaa wa Vuta, Kata ya Kizwite mjini Sumbawanga baada
ya nyumba hiyo kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali baada ya kubaini
kuwa mganga huyo amesababisha vifo vya watoto wawili na mmoja kuwa
mahututi.
IMG_7587 - Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo (kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Vuta Sangu
Sokoni juu ya tukio la kupotea kwa watoto watatu na hatimae kupatikana wawili
wakiwa wamefariki na mmoja kuwa mahututi akiendelea na matibabu.
IMG_7590 -Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo akionyesha eneo katika nyumba iliyokuwa haijamalizika ambapo maiti za
watoto hao zilipatikana baada ya kutupwa na mtuhumiwa James Kapyela ambae ni
mganga wa kienyeji.
IMG_7609 - Diwani wa Kata ya Kizwite ambae
pia ni mchungaji Felician Mavazi (alipiga magoti) akiomba muda mfupi kabla ya
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo kuongea na wananchi wa mtaa huo
wa Vuta kata ya Kizwite juu ya tukio la mauaji ya watoto wawili.
IMG_7623 -Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh.
Joachim Wangabo alipokuwa akiongea na wananchi wa mtaa wa Vuta, Kata ya Kizwite
Sumbawanga mjini.
0 comments:
Post a Comment