METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, March 24, 2019

KAMATI YA KILIMO YAIPONGEZA TARI KWA UTAFITI WA MBEGU BORA, YAITAKA KUTANGAZA TAFITI WANAZOZIFANYA

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti Dkt Christine Ishengoma, ikikagua kitalu nyumba cha kuzalisha mbegu bora za viazi vitamu mara baada ya kutembelea Taasisi ya utafiti wa Kilimo-TARI Kibaha juzi tarehe 22 Machi 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti Dkt Christine Ishengoma, ikikagua kitalu nyumba cha kuangalia na kuthamini magonjwa ya migomba yanayosababishwa na minyoo mara baada ya kutembelea Taasisi ya utafiti wa Kilimo-TARI Kibaha juzi tarehe 22 Machi 2019.
Kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti Dkt Christine Ishengoma, ikikagua maabara ya kusafisha na kuboresha mbegu safi mara baada ya kutembelea Taasisi ya utafiti wa Kilimo-TARI Kibaha juzi tarehe 22 Machi 2019.
Kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti Dkt Christine Ishengoma, ilipotembelea shamba la mihogo mara baada ya kutembelea Taasisi ya utafiti wa Kilimo-TARI Kibaha juzi tarehe 22 Machi 2019.

Na Mathias Canal-Wizara ya Kilimo, Pwani

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imeipongeza Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kwa kufanya tafiti zenye tija na zinazolenga kumbadilisha mkulima wa kawaida ili aweze kupiga hatua kimaendeleo katika kilimo na maisha yake kwa ujumla.

Kamati hiyo imesema kuwa ili kuwezesha wakulima na wafanyabiashara wa Tanzania kuchangamkia fursa ya kilimo cha muhogo, kwani Mei, 2018 ulisainiwa mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya China kuruhusu bidhaa za muhogo mkavu kutoka Tanzania kuingia katika soko la China.

Akizungumza juzi tarehe 22 Machi 2019 mbele ya watumishi wa kituo cha utafiti TARI kilichopo Kibaha Mkoani Pwani Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe Dkt Christine Ishengoma amekipongeza kituo hicho kilicho chini ya Wizara ya Kilimo huku akizitaka Taasisi zote za utafiti nchini kutangaza kazi wanazozifanya.

“Kamati inazitaka Taasisi zote za utafiti wa kilimo nchini kuhakikisha kuwa inatangaza kwenye vyombo vya habari na kwingineko tafiti zao zote ili kulinda kazi kubwa na nzuri wanazozifanya maana kukaa kimya kunafifisha juhudi za kazi zao” Alisisitiza

Dkt Ishengoma alitoa wito kwa Watanzania kuchangamkia fursa ya kilimo hususani kilimo cha muhogo ambacho kimeonesha kuwa na tija kubwa, pia amevitaka vituo vya utafiti wa kilimo viwawezeshe wakulima kupata mbegu bora na mbinu za kisasa ili waongeze uzalishaji na kukidhi mahitaji ya soko hilo.

Katika hatua nyingine mwenyekiti huyo ameihakikishia Wizara ya kilimo kuwa itapitisha Bajeti yote inayohusisha maswala ya utafiti ili kuongeza tija na ufanisi katika kazi ya utafiti.

Alisema sio jambo jepesi kuendeleza kilimo pasina kuwa na tafiti bora hivyo kamati inatambua umuhimu wa utafiti nchini na kwa maana hiyo imeridhia kushirikiana na taasisi hizo za utafiti ili kuwanufaisha wakulima.

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) amekiri sekta ya kilimo haiwezi kuendelea bila kufanya utafiti kuanzia ngazi ya awali ya kilimo kwa kufanyika utafiti wa udongo, mbegu, Mbolea na viuatilifu.

Alisema kuwa Wizara ya kilimo ina mpango wa kupeleka maazimio ya kuwa na sharia ya kulinda tafiti mbalimbali zinazogunduliwa nchini.

Kadhalika, Waziri Hasunga ameungana na kamati hiyo kuitaka TARI kutangaza kazi zake inazozigundua ili zifahamike kuliko kuzifungia ofisini.

Vilevile amewataka watafiti katika vituo vyote vya utafiti kuhakikisha kuwa wanafanya kazi kwa umoja, kutokuwa wabinafsi na kushirikishana kazi zao kwani kufanya kazi kwa ubinafsi kunarudisha nyuma juhudi za maendeleo ya Kilimo.

Mhe Hasunga alisema kuwa “Umefika wakati kila utafiti unaofanywa na wagunduzi wetu uwe una haki miliki kwamba haki ya kazi ya mtaalamu ijulikane na muhusika atambulike ili kusiwe na mtu mwingine wa kuiba tafiti isiyomuhusu”

MWISHO.
Share:

Related Posts:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2025 WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com