Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Shirika la
Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) limetoa mafunzo kwa
watoa huduma za afya kutoka Vituo vya Afya mkoani Mwanza, yanayolenga kuwajengea
uwezo katika kutoa msaada na huduma za kisaikolojia kwa watoto na vijana
wanaoishi na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).
Mafunzo hayo
ya siku tano yalianza jumatatu Machi 25, 2019 hadi Ijumaa Machi 30, 2019 katika
ukumbi wa “Isamilo Lodge” Jijini Mwanza ambapo yamewashirikisha wataalam wa
afya zaidi ya 60 kutoka Halmashauri mbalimbali mkoani Mwanza ikiwemo Nyamagana,
Ilemela, Misungwi, Magu, Ukerewe na Buchosa.
Afisa
Miradi, Huduma Unganishi kwa Jamii kutoka shirika la AGPAHI, Cecilia Yona
amesema mafunzo hayo yatawasaidia watoa huduma za afya katika vituo vya tiba na
matunzo kutambua namna bora ya kuwahudumia wateja wao hususani watoto na vijana.
Amesema
mafunzo hayo yatawasaidia pia kuwatambua watoto na vijana wenye changamoto kisaiklojia
na namna ya kuwasaidia huku wakizingatia upatikanaji wa huduma bora na rafiki kwa
wateja kupitia mbinu mbalimbali ikiwemo michezo.
“Tunatarajia
pia wataenda kuanzisha vikundi vya akina mama wanaoishi na maambukizi ya VVU
ambao wako kwenye kitengo cha kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa
mtoto ili nao waweze kujifunza kupitia uzoefu wao huku vikundi vilivyopo
vikiimarishwa zaidi”. Amesema Yona.
Baadhi ya
washiriki wamesema mafunzo hayo yatawasaidia kuboresha utendaji wao wa kazi
tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo walikuwa wakikumbana na changamoto ya
kutambua mazingira halisi yanayowakabili watoto na vijana kupitia klabu zao.
Shirika la
AGPAHI kwa ufadhili wa Watu wa Marekani kupitia taasisi ya Centres for Disease
Control (CDC), linashirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutekeleza afua mbalimbali za kupambana na
maambukizi ya VVU pamoja na kuwahudumia watu wanaoishi na maambukizi hayo.
Mmoja wa Wawezeshaji, Margaret Safe kutoka Kibaha mkoani Pwani akifafanua jambo kwenye mafunzo hayo.
Mwezeshaji, Margaret Safe akiwasilisha mada kwenye mafunzo hayo.
Afisa Miradi, Huduma Unganishi kwa Jamii kutoka shirika la AGPAHI, Cecilia Yona akizungumza kwenye mafunzo hayo.
0 comments:
Post a Comment