Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai akieleza jambo wakati akifungua Semina kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini( hawapo pichani).
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai (wa pili kulia) akiteta jambo na Waziri wa Madini Doto Biteko (wa pili kushoto)na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dustan Kitandula (wa kwanza kulia). Wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila.
Baadhi ya Watumishi wa Wizara ya Madini, Wenyeviti wa Bodi ya Taasisi chini ya wizara na Wataalam kutoka wizarani na taasisi zake wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa Semina iliyotolewa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai kwa Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na baadhi ya wabunge wa kamati nyingine (hayupo pichani).
Spika
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugani, amesema awali, Taifa halikunufaika
na rasilimali madini kwa kuwa sekta hiyo haikuwa ajenda ya Kitaifa.
“Madini
yaliachwa kwa wabunge ambao rasilimali hiyo inapatikana kwenye maeneo yao, haikuwa
ajenda ya taifa, wengine walizungumzia zaidi masuala yanayowagusa kama korosho,
pamba na mambo mengine, nashukuru tumefanya mabadiliko na sasa matokeo yameanza
kuonekana,” amesema Spika Ndugai.
Amesema
kwa mwelekeo wa sasa, serikali imefika
mahali ambapo manufaa ya rasilimali hiyo yameanza kuonekana kutokana na mageuzi makubwa yaliyofanywa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli na kumpongeza kutokana na
namna anavyohakikisha rasilimali madini inalinufaisha taifa, na kuongeza,
“kilio cha watanzania cha kutokunufaika na madini kimepata mwenyewe, Rais
Magufuli amefanya uthubutu”.
Spika
Ndugai ameyasema hayo Machi 30, 2019, wakati akifungua Semina kwa Wajumbe wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na baadhi ya Wenyeviti wa Kamati
nyingine za bunge wanaohudhuria semina ya siku mbili jijini Dodoma, iliyoandaliwa
na Wizara ya Madini kwa lengo la kutoa elimu ili kupata uelewa wa sekta ya
madini.
Amesema,
awali, ikijulikana kama Wizara ya Nishati na Madini ilikuwa ni kazi hata kwa
bunge hilo kupitisha Bajeti ya wizara hiyo kutokana na kwamba, sekta zote mbili
nishati na madini hazikuwa
zikilinufaisha taifa na kusema, “ kulikuwa na kutokuridhika na sekta zote na
hususan madini, kama taifa tulikuwa hatupati haki yetu tuliyoistahili”.
Kufuatia
hali hiyo, Spika Ndugai amewataka Wabunge
na wananchi kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais Magufuli kwa kuwa
mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa taifa utasaidia kusogeza
mbele maendeleo ya taifa na watu wake.
Aidha,
amewaasa viongozi wote waliobeba dhamana ya kusimamia sekta husika kuhakikisha
wanaichukulia dhamana waliyopewa kwa uzito wa kipekee ili kuliwezesha taifa kufanana na nchi
nyingine ambazo zimeendelea kutokana na rasilimali madini.
Pia,
amepongeza mabadiliko yanayofanywa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na
kueleza kwamba anafurahi kusikia STAMICO mpya tofauti na ilivyokuwa awali.
Akizungumzia
Kamati mbili zilizoundwa na bunge kuchunguza biashara ya madini ya Tanzanite na
Almasi, amesema kuwa, kamati hizo zilifanya kazi nzuri na kwamba bunge litaendelea kuishauri serikali ili kuhakikisha sekta ya madini inazidi kuchangia zaidi katika
uchumi wa taifa.
Ameongeza
kuwa, ripoti hizo zilipokelewa vizuri na serikali na kwamba juhudi zilizochukuliwa
zimewezesha uanzishwaji wa masoko ya madini huku STAMICO ikifanya mabadiliko
makubwa.
Kwa
upande wake, Waziri wa Madini Doto Biteko akizungumza katika semina hiyo,
amesema sekta ya madini ni muhimu kwa
uchumi wa taifa la Tanzania na kueleza kuwa, mchango wa taifa umeendelea
kuongezeka mwaka hadi mwaka na kueleza kuwa, mwaka 2017, sekta hiyo ilichangia
asilimia 4.8 kwenye pato la taifa ikilinganishwa na asilimia 4.0 mwaka 2015.
Akizungumzia
ukuaji wa sekta hiyo amesema umeongeza kwa kasi kutoka asilimia 9.0 mwaka 2015
kufikia 17.5 mwaka 2017, na kusema mafanikio hayo yametokana na juhudi za
serikali kuhakikisha sekta hiyo inachangia zaidi ili kufikia lengo la asilimia 10 ya mchango
wake ifikapo mwaka 2025.
Akizungumzia
marekebisho ya Sheria ya Madini yaliyofanywa mwaka 2017, na usimamizi wa Rasilimali Madini, amesema
umewezesha ongezeko la makusanyo ya maduhuli yatokanayo na shughuli za madini
kutoka Shilingi bilioni 194 iliyotarajiwa kukusanywa mwaka 2017/18 hadi
shilingi bilioni 301.29 sawa na asilimia 154.999 ya lengo la makusanyo kwa
mwaka huo.
“Mhe.
Spika, mwenendo wa ukusanyaji maduhuli kwenye sekta hii kwa mwaka 2018/19 ni wa
kuridhisha ambapo hadi Februari kiasi cha shilingi 218,650,392 kimekusanywa hii
ikiwa ni sawa na asilimia 105.6,” amesema Waziri Biteko.
Ameeleza
kuwa, miongoni mwa sababu zilizopelekea mafanikio hayo ni pamoja na kuongezeka
kwa mrabaha kwa baadhi ya madini,
kuanzisha kodi mpya ya ukaguzi ya asilimia 1; kuimarisha udhibiti
wa utoroshaji wa madini; na kwa kushirikiana na wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama na kuzuia
usafirishaji wa madini ghafi ya nje ya nchi ili
viwanda vya kusafishia na kuongeza ubora wa madini vijengwe nchini.
Akizungumzia
usimamizi wa shughuli za madini ya Tanzanite baada ya kukamilika kwa ukuta unaozunguka
machimbo ya tanzanite Mirerani amesema udhibiti wa madini hayo umeimarika na kusababisha kuongezeka kwa ukusanyaji wa
maduhuli yatokanayo na madini hayo
Ameongeza
kuwa, kufuatia juhudi hizo, ukusanyaji wa maduhuli kutokana na uzalishaji wa
tanzanite kwa wachimbaji wa Wadogo na Kati uliongezeka hadi kufikia shilingi
1,436, 427, 228.99 kwa mwaka 2018,
ikilinganishwa na shilingi 71,861,970
kwa mwaka 2016.
“Uzalishaji
umeongezeka kutoka migodi midogo na ya kati hadi kufikia kilo 781.204 kwa mwaka
2018 ikilinganishwa na kilo 147.7
zilizoripotiwa kwa mwaka 2017 na
kilo 164.6 za mwaka 2016,” amesema Waziri Biteko.
Naye,
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dustan Kitandula,
ameishukuru Wizara kwa kuandaa semina hiyo kwa wabunge na kueleza kuwa, kamati
hiyo itaendelea kupata uelewa kuhusu sekta ya madini.
Mbali na wabunge, wengine wanaoshiriki semina
hiyo ni Wenyeviti wa Bodi za taasisi za zilizo chini ya wizara, Wataalam kutoka
wizarani na taasisi zake.
0 comments:
Post a Comment