Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akipokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Mkoani kagera Godfrey Mheluka alipowasili kwa ajili ya ziara ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia sekta ya ardhi katika mkoa wa Kagera.
Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi vifaa vya kujilinda mmoja wa walemavu wa ngozi katika wilaya ya Karagwe mkoani Kagera katika ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia sekta ya ardhi katika mkoa wa Kagera.
Sehemu ya watu wenye ulemavu wa ngozi katika wilaya ya Karagwe mkoa wa Kagera wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (hayupo pichani) wakati wa kukabidhiwa vifaa vya kujilinda na ngozi na jua.
Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Godfrey Mheluka akizungumza wakati wa kugawa vifaa kwa watu wenye ulemavu wa ngozi wilayani Karagwe mkoa wa Kagera.
Na Munir Shemweta, KARAGWE
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na maendeleo ya Makazi Dkt Angeline
Mabula amewakabidhi vifaa vya kujilinda na ngozi watu wenye ulemavu wa ngozi
katika wilaya ya Karagwe mkoani Kagera.
Dkt Mabula alitoa vifaa hivyo jana baada ya kuombwa na Mkuu wa
Wilaya ya Karagwe Godfrey Mheluka wakati akiwa katika ziara yake ya kuhamasisha
ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia sekta ya ardhi katika wilaya za mkoa wa
Kagera.
Akizungumza wakati wa kugawa vifaa hivyo kwa watu wenye ulemavu wa
ngozi, Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliipongeza wilaya
ya Karagwe kwa kuona uhitaji wa kuwapatia vifaa vya kujilinda.
Alisema, watu wenye ulemavu wa ngozi wana changamoto nyingi lakini
wilaya ya Karagwe imeona umuhimu wa kuwapatia walemavu hao vifaa vya kujikinga
jua na ngozi na kueleza kuwa hilo ni jambo jema linaloweza kuwapa faraja watu
wenye ulemavu.
Aliongeza kwa kusema, uamuzi wa kuwapatia vifaa ni jambo jema na
tayari Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli alishaliona
hilo na katika Baraza lake la kwanza la Mawaziri alimteua mtu mwenye ulemavu wa
ngozi kushika nafasi ya uwaziri.
Kwa mujibu wa Dkt Mabula, kuwa na ulemavu wa ngozi hakumfanyi mtu
mwenye ulemavu huo kushindwa kufanya kazi na kusisitiza kuwa cha msingi ni
kuwawezesha watu wenye ulemavu wa ngozi ili wafanye kazi zao kwa ufanisi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera Godfrey
Mheluka alisema pamoja na Naibu Waziri wa Ardhi kutembelea wilaya yake kwa
ajili ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia sekta ya ardhi
ameona atumie fursa hiyo kuwapatia walemavu wa ngozi vifaa lengo ni kuonesha
kuwajali watu hao.
0 comments:
Post a Comment