METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, March 14, 2019

WAZIRI KAIRUKI AMKABIDHI RASMI WIZARA BITEKO


Waziri wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Angellah Kairuki, akimkabidhi Nyaraka za majukumu ya Wizara ya Madini, Waziri Doto Biteko.Anayeshuhudia katikati ni Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Angellah Kairuki amemkabidhi rasmi Majukumu ya Uwaziri wa Wizara ya Madini, Waziri Doto Biteko katika kikao kilichohudhuriwa na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo.

Waziri Kairuki amemshukuru Waziri Biteko kwa ushirikiano aliompatia kwa kipindi chote alichokuwa Waziri wa wizara hiyo na kueleza kwamba, kabla ya makabidhiano hayo, wamepata wasaa wa kupitia kwa pamoja majukumu na vipaumbele vya wizara ikiwemo maeneo muhimu yanayotakiwa kupewa msukumo.

Naye, Waziri Biteko, akizungumza mara baada ya kukabidhiwa majukumu hayo, amemshukuru Waziri Kairuki na kumwelezea kuwa ni Waziri aliyekuwa mwalimu mzuri kwake kwa kipindi chote alichokuwa Naibu Waziri.

Ameongeza, Waziri Kairuki hakuwahi kumnyima nafasi ya kujifunza ikiwemo kumtuma kutekeleza majukumu mbalimbali nafasi ambayo ilimkomaza.

“ Waziri hakuwahi kuninyima fursa, alinituma popote na nitaendelea kuhitaji ushauri wake katika kutekeleza majukumu yangu,” amesisitiza Biteko.

Makabidhiano hayo yamefanyika Machi 12, ofisini kwa Waziri Biteko Jijini Dodoma.

Waziri Biteko aliteuliwa Januari 8, 2019 kushika wadhifa huo baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kufanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri na kufanya uteuzi wa viongozi mbalimbali. Waziri Biteko alichukua nafasi ya aliyekuwa Waziri wa Madini Angellah Kairuki ambaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com