METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, June 15, 2023

LATRA HUPANGA RATIBA YA MABASI YOTE YA MASAFA MAREFU"NAIBU WAZIRI MWAKIBETE"


 Na Saida Issa, Dodoma

NAIBU Waziri wa Ujenzi na uchukuzi Atupele Mwakibete amesema kuwa Mabasi yote ya masafa marefu hupangiwa ratiba na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ambazo huonyesha stendi za kupakia na kushusha abiria pamoja na muda wa kusimama kwenye stendi hizo.

Naibu Mwakibete ameyasema hayo Leo Bungeni Jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Igunga Nicholas Ngassa alipouliza Je, Serikali inatoa tamko gani kwa mabasi yasiyoingia stendi na ambayo hushusha abiria nje ya Stendi.

"Mheshimiwa Spika, Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicholaus George 
Ngassa, Mbunge wa Igunga kama ifuatavyo:- mabasi ya masafa marefu yamepangiwa kusimama katika Stendi moja tu kwa kila mkoa isipokuwa pale ambapo basi hilo lina abiria anayeshuka katika Stendi ya Wilaya,"amesema Naibu Mwakibete. 

Kadhalika amesema kuwa Utaratibu huo umepangwa ili kuondoa usumbufu na ucheleweshaji wa abiria wa masafa marefu kwa kuwalazimisha kuingia kwenye Stendi hata kama hawana abiria wa kupanda au kushuka. 

"Kwa kuwa Mhe Ngassa anatoka Igunga, naomba kumtaarifu kuwa, stendi ya 
Igunga haimo kwenye Stendi ambazo mabasi ya masafa marefu hulazimika kuingia au kusimama isipokuwa kama yana abiria wa kupanda au kushuka kwenye Stendi hiyo,"amesema. 

Amesema kuwa Stendi hiyo hutumika kwa magari yote yanayotoa huduma ndani ya mkoa wa Tabora na mikoa jirani.

Ameeleza kuwa kwa madereva wanaokaidi kuingia Stendi na kushushia abiria nje ya Stendi hususan barabarani, madereva hao wanakiuka maelekezo ya kifungu cha 50(1) cha Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168 kinachomzuia mtu yeyote kuegesha au kusimamisha gari barabarani bila kujali watumiaji wengine wa barabara, hivyo, wanavunja Sheria. 
Share:

Related Posts:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2025 WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com