Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akivalishwa Scalf na Skauti baada ya kuwasili katika wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera kuanza ziara ya kuhamasisha ukusanyaji maduguli ya serikali kupitia sekta ya ardhi jana
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na wananchi wa halmashauri ya wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera baada ya kutoa hati za ardhi katika halmashauri hiyo katika ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia sekta ya ardhi jana.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akitoka katika Masijala ya Ardhi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera alipokwenda kukagua majalada ya ardhi akiwa katika ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia sekta ya ardhi jana.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza katika Masijala ya Ardhi ya Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera alipokwenda kukagua majalada ya ardhi akiwa katika ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia sekta ya ardhi jana. Wa pili kulia ni Mkuu wa Idara ya Ardhi halmashauri ya Karagwe ambaye pia ni Afisa Ardhi Mteule katika halmashauri hiyo na ile ya Misenyi Benard Esau.
Na Munir Shemweta, KYERWA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline
Mabula amempa wiki moja Mkuu wa Idara ya Ardhi katika Halmashauri ya wilaya ya
Kyerwa mkoani Kagera kuhakikisha anaingiza viwanja 516 katika Mfumo wa Malipo
ya Serikali kwa njia ya Kielektroniki vinginevyo ataondolewe katika wadhifa
huo.
Agizo hilo limafuatia Dkt Mabula kuelezwa na Mkuu huyo wa Idara
kuwa katika halmashauri hiyo jumla ya viwanja 348 pekee ndvyo vilivyoingizwa
katika Mfumo wa Kielektroniki huku viwanja 516 vikiwa havijaingizwa kwenye
mfumo huo.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alitoa agizo
hilo jana tarehe 15 Machi 2019 wakati akiwa katika mfululizo wa ziara yake ya
kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia sekta ya ardhi katika
wilaya za mkoa wa Kagera.
Dkt Mabula alisema kuna uzembe mkubwa kwa Mkuu huyo wa Idara ya
Ardhi ambaye pia ni Afisa Ardhi Mteule wa halmashauri ya wilaya ya Kyerwa
mkoani Kagera kusimamia uingizaji viwanja kwenye mfumo ambao ndiyo unaosaidia
kuongeza mapato ya serikali.
Naibu Waziri alishangazwa na Mkuu huyo wa Idara kushindwa kuingiza
idadi hiyo ya viwanja kwenyea mfumo wa kielektroniki katika kipindi cha mwaka
mzima wakati alieleza kuwa kwa siku moja anao uwezo wa kuingiza viwanja
ishirini.
‘’Kuna uzembe katika kusimamia idara hii ya ardhi na kama mzigo ni
mkubwa kwako kusimamia idara hii basi chagua kuachia nafasi moja katia ya Ukuu
wa idara ya ardhi au Afisa Ardhi Mteule ili uweze kuifanyia nafasi
moja kwa ufanisi’’ alisema Mabula.
Akigeukia suala la utoaji hati katika halmashauri hiyo ya Kyerwa,
Dkt Mabula aliiagiza halmashauri ya Kyerwa kuhakikisha maeneo yote
yaliyochukuliwa kwa ajili ya matumizi ya umma yanapatiwa hati ili kuepuka
migogoro ya ardhi.
Alisema, migogoro mingi kwenye taasisi za umma inasababishwa na
taasisi hizo kutokuwa na hati kwenye maeneo yake na kutolea mfano moja ya
maeneo yanayovamiwa sana ni yale ya wazi na kuzitaka idara husika
kusimamia suala hilo kwa makini.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Rashid Mwaimu alisema
viwanja vingi katika wilaya yake havina hati jambo alilolieleza kuwa wakati
mwingine linawapa ugumu wa kuchukua hatua kwa wamiliki wake ambao aliwaeleza
kuwa wengi wameacha maeneo yao kuwa mapori.
Kwa mujibu wa Mwaimu wilaya hiyo imetoa miezi sita kwa wamiliki
wote wa viwanja ambao hawajaviendeleza na kuviacha mapori kuviendeleza
vinginevyo watafutiwa umiliki wake.
Katika hatua nyingine Dkt Mabula ametaka halamashauri ya wilaya ya
Karagwe mkoa wa Kagera kulitumia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kujenga
nyumba kwa ajili ya watumishi wake ili kuondoa uhaba wa makazi kwa watumishi wa
halmashauri hiyo.
Alibainisha kuwa, hata kama halmashauri hiyo haihitaji nyumba kwa
ajili ya watumishi wake basi inaweza kujengewa nyumba na shirika hilo kwa ajili
ya kuutengeneza mji wa Karagwe na wakati huo kuzitumia nyumba hizo kama
rasilimali ambapo nyumba hizo zinaweza kupangishwa na kuiwezesha
halmashauri kujipatia kipato.
‘’Halmashauri badala ya kutegemea kuingiza mapato katika baadhi ya
vyanzo kama vile kituo cha mabasi wanaweza kulitumia shirika la nyumba kuongeza
hadhi ya mji na mapato kwa halmashauri’’ alisema mabula.
0 comments:
Post a Comment