Naibu Waziri wa kilimo, Mhe. Omary Mgumba akitembelea moja ya shamba la mfano la pamba katika Kata ya Mwabusalu Wilayani Meatu, wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi wilayani humo
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba nchini, Marco Mtunga akitoa maelezo juu ya namna pamba inavyopaswa kuhudumiwa wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa kilimo, Mhe. Omary Mgumba katika Kata ya Mwabusalu Wilayani Meatu.
Naibu Waziri wa kilimo, Mhe. Omary Mgumba akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Mwabusalu wilayani Meatu, wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi wilayani humo.
Sehemu ya shamba la pamba la mfano lililopo katika Kijiji cha Mwabusalu kata ya Mwabusalu wilayani Meatu Mkoani Simiyu.
Naibu Waziri wa kilimo, Mhe. Omary Mgumba amewataka
wakulima wa pamba kata ya Mwabusalu wilayani meatu Mkoani Simiyu
iliyochaguliwa kuzalisha mbegu za pamba kuzingatia kanuni za kilimo bora lengo
likiwa kupata mbegu bora zitakazotumika katika maeneo yanayolima zao hilo hapa
nchini.
Ameyasema hayo akiwa kwenye ziara ya kikazi
wilayani hapo yenye lengo la kukagua shughuli za kilimo, kusikiliza kero
za wakulima katika kujiletea maendeleo wakati akiongea kwenye mkutano wa
hadhara uliofanyika kwenye kata ya mwabusalu iliyopo wilayani hapo.
Awali akimkaribisha Naibu Waziri wa Kilimo Mgumba,
Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Dkt. Joseph Chilongani amesema kuwa bado
wanaendelea kutoa elimu kwa wakulima waliopewa dhamana ya kuzalisha mbegu za
pamba kutochanganya mazao huku akiongeza kuwa mbegu hiyo itazalishwa ya
kutosha.
“Mbegu inazalishwa hapa Mwabusalu na baadaye
inapelekwa maeneo mengine yanayolima pamba nchini, isingependeza kukawa na
maotea kwenye eneo ambalo limepewa dhamana ya kuzalisha mbegu, tunaendelea
kuwaelimisha wakulima na kuhakikisha kuwa maotea yasiwe sehemu ya pamba
itakayonunuliwa kwa ajili ya mbegu” alisema Dkt. Chilongani.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mkuu wa Bodi ya Pamba
nchini, Marco Mtunga amemuomba Mkuu wa Wilaya ya Meatu na Kamati
yote ya Ulinzi na Usalama isimamie operesheni ya kuondoa maotea kwenye mashamba
ya pamba iliyokuwa imesitishwa ili kulinda ubora wa mbegu na mfumo wa kuzalisha
mbegu za pamba.
“Tulikuwa tunaendesha operesheni ya kuhakikisha
mashamba yote ya kuzalisha mbegu hapa Mwabusalu yanazingatia taratibu za
kuzalisha mbegu, ilisitishwa kutokana na vitisho vya wana Mwabusalu kutaka
kuwapiga waliokuwa wakipita kwenye mashamba kuondoa maotea, Mhe. DC kuanzia
kesho Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya isimamie zoezi hili ili tusipoteze
mfumo wa kuzalisha mbegu bora” alisema Mtunga”
Baadhi ya wakulima wa pamba katika Kata ya
Mwabusalu wameiomba Serikali kuendelea kuwapata pembejeo kwa wakati na kutoa
wito kwa viongozi wa kisiasa kuwaongoza katika kuzingatia kanuni za kilimo bora
badala ya kuwapotosha ili waweze kulima kwa tija na kutoka kwenye
umaskini.
“Ninaomba Serikali iendelee kutoa madawa na mbolea
kwa wakati ili tuweze kuzalisha kwa tija maana mwaka huu tumeongeza uzalishaji
na tunatarajia mavuno mengi kwa kuwa pamba haijashambuliwa sana na wadudu kama
mwaka jana” alisema Charles Thomas mkulima Mwabusalu
“Baadhi ya viongozi wa kisiasa waache kuhubiri
habari mbaya kwenye kilimo cha pamba maana hawahubiri suala la kufuata
sheria, mfano wanapotuambia tuchanganye pamba na mazao mengine wakati wataalam
wanasema haitakiwi je wanatusaidia kutoka kwenye umaskini au wanataka tuendelee
kuwa maskini” alisema Bupolo Mahangi
Akijibu baadhi ya hoja zilizoibuliwa kwenye mkutano
huo Naibu Waziri Mgumba amewataka baadhi ya wanasiasa kuwa sehemu ya kutoa
elimu na kuwaongoza wakulima hao kuzingatia kanuni za kilimo bora ili waweze
kulima kwa tija, kuzalisha mbegu bora na kuongeza mavuno.
Naibu Mgumba jana amemaliza ziara yake ya
kikazi ya siku mbili mkoani Simiyu kwa kutembelea mradi wa kilimo cha
umwagiliaji, kutembelea mashamba ya pamba na kuzungumza na wananchi wilayani
Maswa, akiwa wilaya Meatu alitembelea shamba la kuzalisha mbegu za pamba na
kuzungumza na wananchi wa eneo hilo la Mwabusalu lililopo wilayani hapo.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment