Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula (katikati), Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (wa kwanza kushoto) na Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Manonga, Seif Gulamali (wa Pili kulia) wakimsikiliza mtaalam kutoka kampuni ya ubia ya Arab Contractors na Elsewedy Electric wakati akizungumzia mradi wa umeme wa Rufiji (MW 2115).
Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga (kushoto) na Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dkt Tito Mwinuka (katikati) wakikagua eneo kutakapotekelezwa mradi wa umeme wa Rufiji (MW 2115), wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, (katikati), akizungumza na Wataalam wanaosimamia na wanaotekeleza mradi wa umeme wa Rufiji (MW 2115) mara baada ya kufika katika eneo la mradi huo akiwa ameambatana na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
Moja ya nyumba inayojengwa na mkandarasi anayetekeleza mradi wa umeme wa Rufiji ambapo katika eneo hilo kunajengwa kambi ya muda ya Wafanyakazi wa mradi huo.
Na Teresia Mhagama, Pwani
Imeelezwa kuwa, kazi mbalimbali za
maandalizi ya ujenzi wa mradi wa umeme wa Rufiji ( MW 2115) zinazofanywa na
Mkandarasi kampuni ya ubia ya Arab Contractors na Elsewedy Electric
zimefikia zaidi ya asilimia 4O.
Hayo yalielezwa na Waziri wa
Nishati, Dkt Medard Kalemani wakati alipokuwa akitoa taarifa ya mradi huo kwa
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambao walitembelea
eneo la mradi lililopo wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani.
Kamati hiyo ya Bunge pia ilikagua
miundombinu wezeshi iliyotekelezwa na Serikali ikiwemo Barabara, umeme,
nyumba za Wafanyakazi na sehemu maalum ya kushushia mizigo katika Stesheni ya
Tazara katika Kituo cha Fuga.
Dkt. Kalemani, alisema kuwa,
Mkandarasi huyo ameanza kazi za maandalizi mara baada ya kukabidhiwa eneo hilo la
mradi mwezi wa Pili mwaka huu.
Alisema kuwa, miongoni mwa kazi
ambazo Mkandarasi anaendelea kutekeleza kwa sasa ni ujenzi wa kambi ya
muda ya Wafanyakazi, uletaji wa vifaa na mitambo itakayotumika wakati wa ujenzi
pamoja na kazi za kuchukua sampuli za udongo na maji kwa ajili ya utafiti.
Aliongeza kuwa, mara baada ya
kukamilisha kazi hizo za maandalizi Mkandarasi huyo anatakiwa kumaliza kazi ya
ujenzi ndani ya miezi 36.
Alieleza kuwa, pamoja na kuridhishwa
na hatua hiyo ya maandalizi, bado Serikali kupitia Wizara ya Nishati itaendelea
kumsimania mkandarasi ili amalize kazi ndani ya muda uliopangwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
Kamati ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula, baada ya kukagua
miundombinu iliyotekelezwa na Serikali pamoja na kazi za maandalizi
zinazofanywa na Mkandarasi, aliipongeza Serikali kwa kuamua kuutekeleza mradi
huo na kuusimamia kikamilifu.
Alisema kuwa, Kamati hiyo pia
inafuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili uweze kukamilika kwa wakati
kutokana na umuhimu wake nchini ambapo pia alitoa wito kwa Wizara kutorudi
nyuma katika usimamizi wa mradi.
Pia, alitoa wito kwa wafanyabiashara
hapa nchini kuchangamkia fursa zinazopatikana katika mradi kwani Serikali
itatumia takribani shilingi Trilioni 6.5 kutekeleza mradi huo hivyo ni muhimu
watanzania wafaidike na fedha hizo.
Katika ziara hiyo, viongozi
mbalimbali waliambatana na Kamati hiyo akiwemo Kaimu Kamishna wa Umeme na
Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt
Tito Mwinuka pamoja na wataalam kutoka kampuni inayotekeleza mradi huo.
0 comments:
Post a Comment