METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, March 1, 2019

Katibu Mkuu Kilimo amkaribisha Katibu Mkuu wa Kilimo wa Ujerumani kwenye ASDP II


Katibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo (Tanzania) Mhandisi Mathew Mtigumwe akizungumza na Mgeni wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Chakula (Ujerumani) Bwana Michael Stubgen katika mkutano wao wa leo tarehe 1 Machi 2019 katika ukumbi wa Wizara ya Kilimo Dodoma
 Katibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo (Tanzania) Mhandisi Mathew Mtigumwe akizungumza na Mgeni wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Chakula (Ujerumani) Bwana Michael Stubgen sambamba na ujumbe kutoka nchi hizo mbili katika mkutano huo katika ukumbi wa Wizara ya Kilimo Dodoma
Katibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo (Tanzania) Mhandisi Mathew Mtigumwe akimkabidhi Mgeni wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Chakula (Ujerumani) Bwana Michael Stubgen nakara za vitabu vya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo (ASDP II) baada ya kumaliza mkutano wao wa leo

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo (Tanzania) Mhandisi Mathew Mtigumwe amemkaribisha Katibu Mkuu mwenzake wa Wizara ya Kilimo na Chakula (Ujerumani) Bwana Michael Stübgen ili nchi yake iwekeze katika maeneo mbalimbali ya Sekta ya Kilimo hususani kwenye Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo (ASDP II).

Awali Mhandisi Mathew Mtigumwe amesema Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo imeanza kutekelezwa June mwaka 2018 kwa pamoja kati ya Serikali, Wabia wa Maendeleo pamoja na Sekta binafsi ambapo jumla ya Shilingi Tilioni 13 zinataraji kuwekezwa kwa ajili ya kuleta mapinduzi ya kweli kwenye Sekta ya Kilimo Mifugo na Uvuvi.

Mhandisi Mtigumwe amemwambia Mgeni wake huyo kuwa maeneo kadhaa ambayo Ujerumani inaweza kuisaidia Tanzania wakati wa kuitekeleza Programu ya ASDP II ni pamoja na eneo la utafiti katika kilimo, usalama wa chakula (ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya uhifadhi wa chakula hususan i mazao ya nafaka/lishe) pamoja na eneo la pembejeo za kilimo hususani ujenzi wa viwanda vya kutengeneza mbolea hapa nchini ili ipatikane kwa bei nafuu na kwa wakati.

Mhandisi Mtigumwe amemwambia Mgeni wake huyo kuwa kimsingi Programu ya ASDP II imeandaliwa kwa lengo la kujibu matatizo ya Mkulima wa Tanzania kuanzia anapoanza kulima mpaka anapofika kwenye hatua ya kupata masoko ya mazao yake baada ya kuvuna kwa kuangalia mnyororo wa thamani (Value chain).

Naye Katibu Mkuu wa Wizara Kilimo na Chakula (Ujerumani) Bwana Michael Stübgen amemwambia Mwenyeji wake huyo kuwa nchi yake inatambua juhudi ambazo zimekuwa zikifanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika maendeleo ya Sekta ya Kilimo na kuongeza kuwa wapo tayari kuendeleza mahusiano mazuri yaliyopo baina ya nchi hizi mbili.

Bwana Michael Stübgen amesema licha ya kuwa Taifa la Ujerumani limeendelea kuliko Tanzania lakini linakabiliwa  na changamoto ya watu wake kupata utapiamlo na kunenepa kupita kiasi na kuongeza kuwa ni wakati muafaka kwa nchi hizo mbili kuungana pamoja katika kukabiliana na changamoto hizo.

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com