Baadhi ya mitambo ya umeme katika
kituo cha kupoza umeme cha Makambako mkoani Njombe ambacho kimejengwa kupitia
mradi wa umeme wa Makambako- Songea.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard
Kalemani (wa pili kushoto) akiongoza Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Nishati na Madini kutembelea kituo cha kupoza umeme cha Makambako mkoani
Njombe. Wa Pili kulia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mariamu Ditopile Mzuzuri na
Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard
Kalemani (wa kwanza kushoto) akitoa maelezo kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Nishati na Madini wakati walipotembelea kituo cha kupoza umeme cha
Makambako mkoani Njombe. Wa Pili kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mariamu
Ditopile Mzuzuri.
Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga
(aliyenyoosha mkono) akitoa maelezo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na
Madini kuhusu kituo cha kupoza umeme cha Songea ambacho kimejengwa kupitia mradi
wa umeme wa Makambako-Songea. Wa Pili kulia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo,
Mariamu Ditopile Mzuzuri
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati
na Madini, chini ya Mwenyekiti, Mariamu Ditopile Mzuzuri, imeipongeza Serikali
kwa kutekeleza mradi wa umeme wa Makambako- Songea (kV 220) ambao umewezesha
Mikoa ya Ruvuma na Njombe kupata umeme wa uhakika kutoka Gridi ya Taifa.
Kamati hiyo, imetoa pongezi hizo
wilayani Songea, Mkoa wa Ruvuma, baada ya kukagua utekelezaji wa
mradi huo ambao umehusisha ujenzi wa njia ya umeme ya msongo kV 220 kutoka Makambako
hadi Songea, ujenzi wa Vituo vya kupoza umeme vya Makambako, Madaba na Songea
na usambazaji umeme katika Vijiji 122.
Kabla ya kukagua kituo cha
kupoza umeme cha Songea, Kamati hiyo ilikagua vituo vya Makambako na Madaba
pamoja na njia ya usafirishaji umeme kutoka Makambako hadi Songea ambapo
watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO), walihudhuria.
Pamoja na pongezi hizo, Mwenyekiti wa
Kamati hiyo, aliiagiza Wizara pamoja TANESCO kuhakikisha kuwa, wanapeleka umeme
katika Vijiji vyote vilivyopangwa kupelekewa umeme kupitia mradi huo na
kutoruka kijiji chochote ambacho kimepitiwa na mradi.
Aidha, aliiagiza Wizara ya Nishati na
TANESCO kuhakikisha kuwa, inahamasiha wananchi kutumia umeme huo kwa matumizi
mbalimbali ikiwemo ya viwandani kwani mikoa hiyo sasa ina umeme wa kutosha na
wa uhakika na Serikali inahitaji wateja wengi zaidi ili kuongeza mapato.
Awali, katika kituo kupoza umeme cha
Makambako, Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani aliieleza Kamati hiyo kuwa,
mradi huo umekamilika mwaka 2018 na kazi inayoendelea sasa ni usambazaji wa
umeme katika Vijiji vya awali 122 ambapo Vijiji 105 tayari vimeshaunganishwa na
nishati hiyo.
Dkt. Kalemani aliongeza kuwa, mradi
huo umetekelezwa na Serikali ya Tanzania kupitia TANESCO kwa
kushirikiana na Serikali ya Sweden kupitia Shirika la Maendeleo la Sweden
(Sida) ambapo jumla ya gharama za mradi ni shilingi bilioni 216 na jumla ya
wateja wa awali 22,000 watafaidika na mradi huo.
Kwa upande wake, Kaimu Kamishna wa
Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, alisema kuwa, miundombinu
hiyo ya usafirishaji umeme (kV 220) imejengwa kwa umbali wa kilomita 250 na
jumla ya nguzo (Tower erection) 711 zimesimikwa.
Aliongeza kuwa, kufika kwa umeme wa
Gridi katika mikoa hiyo, kumefanya wananchi wahamasike kutumia umeme huo na
kutoa mfano kuwa, awali matumizi ya umeme kwa Mkoa wa Ruvuma
yalikuwa ni takriban megawati 9 lakini sasa yameongezeka na kufikia megawati 11
huku kazi ya kuwasambazia umeme wananchi ikiendelea.
0 comments:
Post a Comment