METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, March 29, 2019

HAKUNA ZUIO KUUZA NAFAKA NJE YA NCHI-MHE MGUMBA

Naibu waziri wa Kilimo Mhe Omari Mgumba (Mb)

Na Bashiri Salum, Wizara ya kilimo- Arusha

Naibu waziri wa Kilimo Mhe Omari Mgumba (Mb) leo tarehe 29 Machi 2019 amekanusha vikali taarifa zilizoandikwa na gazeti la kila siku hapa nchini la The citizen la tarehe 28 machi 2019 lililoandika kwamba Serikali imezuia kuuza mazao ya nafaka kuuza nje ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa kituo cha utafiti Seliani (TARI Seliani) Jijini Arusha, Mhe Mgumba amesema kuwa alipigiwa simu na gazeti hilo wakitaka kujua hatua za serikali dhidi ya taarifa ya uwepo wa hali ya ukame unaosababishwa na kuchelewa mvua kunyesha.

“Taarifa hiyo sio ya kweli kwa sababu serikali kupitia wizara ya kilimo imetafuta masoko ya wakulima katika nchi mbalimbali ikiwemo Burundi, Rwanda, Sudani na Zambia lengo likiwa ni kuwapatia soko la uhakika wakulima wa mazao ya nafaka na mazao mengine” Alikaririwa Mhe Mgumba na kuongeza kuwa

 “Kwa kipindi kirefu baadhi ya mazao ya nafaka yalikuwa hayana soko tumefanya juhudi kuwapatia soko la mazao ya nje ya nchi, hivyo haiingii akilini kuwazuia wakulima kuuza mazao yao haiwezekani

Mhe Mgumba alibainisha kuwa taarifa iliyotolewa na Gazeti la kila siku la The Citizen yenye kichwa cha habari kisemacho "DROUGHT ALERT STOPS PLAN TO EXPORT EXCESS FOOD STOCKS" imetoa taswira ya tofauti kutokana na mahojiano yaliyofanywa kati yake na gazeti hilo.

Mhe Mgumba asisitiza kwamba serikali haijapiga marufuku usafirishaji na uuzaji wa mazao ya kilimo nje ya nchi na haina mpango wa kuweka katazo hilo ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa soko la wakulima kwa kuwa Taifa lina chakula cha kutosha.

Aidha, ametoa wito kwa wakulima na wafanya biashara wanaojishughulisha na kununua au kuuza mazao ya kilimo kuendelea na biashara yao  ili kuongeza tija kwa wakulima.

Katika mkutano huo  Naibu waziri Mhe. Omary Mgumba amewataka wakulima kuendelea kuchangamakia fursa za masoko ya ndani na nje ya nchi ambazo zina upungufu au uhitaji wa mazao hayo.

Kufuatia taarifa za mamlaka ya hali ya hewa na shirika la chakula duniani iliyohusu uwezekano wa kuwepo kwa ukame maeneo mengi ya nchi serikali imetuma wataalamu meneo mbalimbali ya nchi  kufanya  tathmini ya hali hiyo ili kuona namna bora ya kupunguza madhara ambayo yanaweza kutokea alibainisha Mhe Mgumba.

Hata hivyo Mhe amewataka wakulima kuchukua tahadhari  na hali hiyo kwa kuhakikisha kwamba wanabakiza akiba ya chakula cha kutosha familia zao wakati ukame ukitokea .

Aidha, alisema kuwa jukumu kubwa la serikali ni kuhakikisha kwamba taifa linajitosheleza kwa chakula na kilimo kinaendelea kutoa ajira kwa watanzania walio wengi.

MWISHO.
Share:

Related Posts:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2025 WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com