Waziri wa Madini Doto Biteko akiwa na Viongozi wa Kampuni ya Acacia wa mgodi North Mara, ofisini kwake jijini Dodoma.
Waziri wa Madini Doto Biteko akiwa na Viongozi wa Kampuni ya Acacia wa mgodi North Mara, ofisini kwake jijini Dodoma. Kulia ni Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Mara, Agness Marwa.
Na Issa Mtuwa, Dodoma
Uongozi
wa Kampuni ya Acacia kupitia Mgodi wa North Mara umezungumza na Serikali
kuelezea hatua zilizochukuliwa hadi sasa kudhibiti maji yenye sumu ikiwa ni
wiki moja tu ipite tangu Waziri wa Madini Doto Biteko, atangaze kufunga shughuli
za mgodi huo endapo utashindwa kudhibiti maji ya sumu yanayotiririka kwenye makazi
ya watu, ifike Machi 30 mwaka huu.
Tamko
hilo la serikali limeifanya kampuni ya Acacia kuchukua hatua za haraka za
kudhibiti maji hayo ili kukwepa rungu la serikali la kuufunga mgodi huo. Machi 12, uongozi wa Acacia North Mara ulikutana
na Waziri Biteko ofisini kwake jijini Dodoma kwa lengo la kueleza hatua
iliyofikiwa ya kutekeleza agizo la serikali.
Uongozi
wa kampuni hiyo ukizungumza katika kikao hicho, ulieleza kuwa, tayari mgodi huo
umechukua hatua za haraka tangu kutolewa kwa agizo na kwamba hadi sasa suala la
kudhibiti maji yenye sumu limeshetekelezwa na hakuna maji yanayotiririka
kuelekea kwenye makazi ya watu.
Aidha,
ulimweleza kuwa, pamoja na kudhibiti maji hayo kupitia bwawa la kuhifadhia maji
yenye sumu yajulikanayo kitaalam kama “topesumu” (Tailings Storage Facility-
TSF) mgodi umeanza kuchukuwa hatua za kujenga TSF mpya.
“Mhe.
Waziri tumekuja kutoa mrejesho wa utekelezaji wa agizo lako, tunafurahi
kukuambia kuwa tumetekeleza agizo hilo na kwa sasa hakuna maji yanayotiririka. Pamoja
na hatua hiyo mgodi umeanza mchakato wa ujenzi wa bwawa jipya (TSF) la kuhifadhia topesumu,”
walieleza.
Aidha,
ulimweleza Waziri Biteko kuhusu hujuma za uharibifu wa miundombinu ya bomba la
maji yenye sumu unaofanywa kwa maksudi na wakazi wanaozunguka mgodi ili
kufifisha juhudi zao za kudhibiti maji hayo wakiwa na lengo la kuufanya mgodi
uonekane haujachukuwa hatua kudhibiti jambo hilo, ambapo walionesha picha
mbalimbali ya namna bomba lilivyo pasuliwa ili maji yatiririke kuelekeka kwa
wananchi.
Akizungumza
katika kikao hicho, Waziri Biteko alieleza kuwa, amepokea taarifa ya kampuni
husika na kuwapongeza kwa hatua zilizochukuliwa na kusema kuwa, ukweli wa jambo
hilo atauthibitisha mara baada ya kupata ripoti ya wataalam watakaokwenda
kuhakikisha kuhusu utekelezaji wa agizo hilo na kuongeza,“katika hili sitanii
juu ya kuufunga mgodi ikiwa utashindwa kudhibiti tope sumu,”.
“Naomba nirudie tena katika hili sitanii, sitabadilisha
msimamo wangu kama serikali na utaendelea kubaki pale pale dawa pekee ni
kutekelezwa kwa agizo hilo. Lakini niseme ukweli, nasikitishwa sana na kitendo
hiki cha wananchi kupasua bomba, kwa hili sikubaliani nao na siwaungi mkono.
Pia, aliongeza kuwa, atawasiliana na Mkuu wa
Mkoa na Mkuu wa Wilaya kuona namna ya kudhibiti hali hiyo ili wale watakao
bainika wachukuliwe hatua.
Waziri
Biteko alilitoa agizo hilo Machi 6, alipoutembelea mgodi huo hapo kwa
ziara ya kikazi pamoja na kuzungumza na wananchi
kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Nyamongo wilaya ya Tarime.
0 comments:
Post a Comment