METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, March 14, 2017

Mbarawa: Wekeni mikakati kudhibiti ajali

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amewataka wadau wa usafirishaji kuweka mikakati thabiti ya kupunguza ajali za barabarani nchini ili kuokoa maisha ya Watanzania.

Aliyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano Maalumu wa Kanda wa kujadili na kutathmini changamoto za usalama barabarani na jinsi ya kuzikabili uliowashirikisha wadau mbalimbali wa usalama barabarani kutoka ndani na nje ya nchi.

Alisema ajali za barabarani zimekuwa zikikatisha maisha ya Watanzania wengi wakiwamo vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa, hivyo ni jukumu la wadau kuondoa hali hiyo.

“Kama tukijifunza vizuri na kuyafanyia kazi mafunzo haya tunaweza kubadili hali ya usalama barabarani kwani inaumiza kuona vifo vya watu wengi vinavyotokana na ajali za barabarani hivyo ni wakati wa Jeshi la Polisi, na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) kushirikiana kukomesha ajali hizi,” alisema.

Mwenyekiti wa Mfuko wa Barabara Tanzania (RFB), Joseph Haule alisema Bodi hiyo inashirikiana na taasisi nyingine katika kuhakikisha miundombinu ya barabara inakuwa salama na kupitika wakati wote.

Alisema kama jitihada madhubuti hazitachukuliwa kwa haraka inakadiriwa kwamba vifo vinavyotokana na ajali vinaweza kuongezeka kwa asilimia sita kwa mwaka kutokana na kuongezeka kwa vyombo vya moto huku akisema wanaume ndiyo waathirika wakubwa wa hilo.

Mapema Mwenyekiti wa Shirikisho la Kimataifa la Barabara (IRF), Kiran Kapila alisema zaidi ya Dola za Marekani trilioni 1.8 zinapotea kila mwaka kutokana na ajali za barabarani na kuziomba serikali kuchukua hatua kukabiliana na tatizo hilo.
Share:

Related Posts:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2025 WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com