METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, February 18, 2019

Waziri wa Nishati, azindua Bodi mpya ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na kutoa maelekezo

Baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambayo imezinduliwa na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (katikati) akizungumza wakati wa uzinduzi wa  Bodi mpya ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA). Katika kikao hicho pia walihudhuria Watendaji wa Wizara ya Nishati na Wakala wa Nishati Vijijini (REA). Kulia kwa Waziri ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, leo amezindua Bodi mpya ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), na kutoa maelekezo mbalimbali kwa Bodi hiyo yatakayopelekea kazi ya usambazaji umeme vijijini kufanyika kwa kasi na ufanisi.
Kikao cha Waziri na Bodi hiyo kimefanyika jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua, Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Wizara ya Nishati, Raphael Nombo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga na watendaji wengine kutoka Wizara na REA.
Akizungumza na Bodi hiyo, Dkt Kalemani alieleza sababu mbalimbali za  kuvunjwa kwa Bodi iliyopita tarehe 12 Novemba, 2018 kuwa ni kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kushindwa kusimamia vizuri Wakala wa Nishati Vijijini.
“ Leo tunawakabidhi majukumu yenu lakini suala la msingi ni kuwatumikia wananchi kwani tunawajibika kwao hivyo yaliyotokea kwenye Bodi iliyopita, yasitokee kwenye Bodi yenu”. Alisema Dkt Kalemani
Alitaja majukumu ya Bodi hiyo kuwa ni kusimamia Wakala wa Nishati Vijijini ili utekeleze majukumu yake kwa ufanisi na weledi na kusimamia shughuli za Wakala  ili zifanyike kwa malengo na Dira ya Serikali ya kusambaza umeme katika Vijiji vyote nchini.
Aliongeza kuwa, majukumu mengine ya Bodi hiyo ni kusimamia Fedha za Mfuko wa Nishati Vijijini ili tija yake ionekane na kuitaka Bodi hiyo kutokuwa chanzo cha migogoro inayoweza kuchelewesha au kukwamisha kazi za Wakala.

Aidha, ameiagiza Bodi hiyo kuharakisha utekelezaji wa kusambaza umeme katika Vijiji, vitongoji na miradi mbalimbali ya kijamii na kuwasimamia ipasavyo wakandarasi wa umeme vijijini ili kazi zao ziende kwa haraka kwani wengi wao hawafanyi kazi zao inavyotakiwa.
Dkt. Kalemani amezindua Bodi hiyo baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli kumteua Bw. Michael Nyagoga kuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo tarehe 14 Februari 2019.
Wajumbe wa Bodi hiyo ni Oswald Urassa, Mhandisi Styden Rwebangila, Francis Songela, Louis Accaro, Dailin Leonard, Henry Mwimbe na Dkt. Andrew Komba.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com