METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, February 10, 2019

WAZIRI MKUU ATOA SIKU 21 KWA VIWANDA VYA VILEO


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisoma hotuba  ya kuahirisha Bunge jijini Dodoma, Februari  9, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa siku 21 kwa viwanda vyote vinavyozalisha vileo nchini viwe vimefunga mfumo ukusanyaji kodi kwa kutumia stempu za kielektroniki.

Pia ameziagiza Wizara na Taasisi zote za Umma ziwe zimejiunga na Mfumo wa Serikali wa Kielektroniki wa ukusanyaji na usimamizi wa maduhuli (GePG) kabla ya Juni mwaka huu.

Ametoa maagizo hayo leo (Jumamosi, Februari 9, 2019) , wakati akiahirisha mkutano wa kumi na nne wa Bunge la kumi na moja, Bungeni jijini Dodoma.

Waziri Mkuu amesema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) isimamie uwekaji wa mifumo hiyo na ifikapo februari 28, 2019 kila kiwanda kiwe kimefunga mfumo huo.

“Naielekeza TRA kusimamia uwekaji wa mifumo ya kukusanya kodi za vileo kwa kutumia stempu za kielektroniki kwa viwanda vyote vinavyozalisha vinywaji hivyo.”

Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuongeza mapato na kuimarisha usimamizi wa matumizi ya fedha na rasilimali za umma ili kufikia malengo.

Miongoni mwa mikakati hiyo ni kutumia mfumo wa kielektroniki wa stempu za kodi kwenye viwanda vinavyozalisha bidhaa zinazotozwa ushuru wa bidhaa na zile zinazoingizwa nchini. 

Waziri Mkuu amesema mfumo huo utasaidia Serikali katika kupata taarifa sahihi za uzalishaji na kupunguza uvujaji wa mapato ya Serikali.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kutekeleza maelekezo ya Rais Dkt. John Magufuli aliyoyatoa Januari 22, 2019, alipokutana na wadau wa sekta ya madini. 

AmesemaSerikali imefutaKodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na Kodi ya Zuio ya asilimia  tano ya mwisho inayotozwa kwenye bei ya kuuzia madini ya aina zote kwa wachimbaji hao. 

Waziri Mkuu amesema hatua hiyo inatarajiwa kupunguza utoroshwaji wa madini; kuwatambua wachimbaji wadogo kupitia masoko ya madini yatakayoanzishwa.

Pia itasaidia kuwapunguzia gharama wachimbaji wadogo na hivyo kuendesha shughuli zao kwa ufanisi pamoja na kuongeza wigo wa mapato kwa kuwa madini yatauzwa ndani ya nchi. 

Nitoe rai kwa wachimbaji wote wadogo kushirikiana na Mamlaka mbalimbali za Serikali kutekeleza maazimio yaliyofikiwa katika kikao na Mheshimiwa Rais.”

Amesema siku zote Watanzania wanamuenzi Rais Dkt. John Magufuli, kwa hatua za makusudi anazochukua katika kuhakikisha anaimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato.

Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Magufuli anafanya hayo yote kwa lengo la kuona Tanzania inapunguza utegemezi wa misaada kutoka katika mataifa mengine.

“Mifano maelekezo aliyoyatoa kwa Mawaziri, Wakuu wa Mikoa wawasilishe mapendekezo kuhusu namna bora ya kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani katika maeneo yao.”

Waziri Mkuu amesema tayari Serikali imeshapokea mapendekezo hayo na imetoa maagizo mahsusi kwa TRA na TAMISEMI zishirikiane katika ukusanyaji wa kodi za majengo.

Akizungumzia kuhusu hali ya uchumi, Waziri Mkuu amesema imeendelea kuimarika, ambapo kati ya Januari hadi Septemba 2018, pato la Taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 6.7 ikilinganishwa na asilimia 6.2 katika kipindi kama hicho mwaka 2017. 

AmesemaOngezeko hilo la ukuaji wa uchumi limechochewa zaidi na uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu hususan ujenzi wa barabara, reli na viwanja vya ndege.

Waziri Mkuu amesema masuala mengine yaliyochangia ukuaji mzuri wa uchumi ni kutengemaa kwa upatikanaji wa nishati na hali nzuri ya hewa kwa upande wa kilimo.

“Shughuli za kiuchumi zilizoendelea kutoa mchango mkubwa katika pato la Taifa kwa kipindi hicho ni kilimo (asilimia 33.4), ujenzi (asilimia 15.7) na biashara (asilimia 10.2).”

Amesema kutokana na umuhimu wa sekta ya kilimo, Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya umwagiliaji, kuhakikisha pembejeo za kilimo zinapatikana kwa wakati.

Pia kuhakikisha huduma za ugani zinaimarishwa katika maeneo yote nchini pamoja na  kuboresha upatikanaji wa miundombinu ya hifadhi na masoko. 

Lengo la Serikali ni kuongeza tija kwenye uzalishaji wa mazao ya kilimo na hivyo kumwongezea kipato mkulima kitakachomwezesha kujikimu na kujikwamua na umaskini.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com