Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya
Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) Dkt. Stephen Nindi akitoa mada wakati wa
warsha ya ushirikishwaji wa wananchi katika upangaji, usimamizi na utekelezaji
wa mipango ya matumizi ya ardhi nchini.
Mwanafunzi wa mwaka wa pili Ngeze
Valentina wa kozi ya RDP akichangia mada wakati wa majadiliano juu ya
ushirikishwaji wa wananchi katika upangaji, usimamizi na utekelezaji wa mipango
ya matumizi ya ardhi.
Mshiriki wa warsha Kiteri Sophia kutoka
Chuo Kikuu cha Ardhi akitoa maoni yake juu ya ushiriki wa wanawake katika hatua
za upangaji wa mipango ya matumizi ya ardhi.
Baadhi ya washiriki wa warsha wakifuatilia
kwa makini mada zilizokuwa zikitolewa wakati wa warsha ya upangaji, usimamizi
na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi.
Tume ya Taifa ya Mipango
ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa kushirikiana na Taasisi ya Lantmateriet ya
nchini Sweden kupitia ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Sweeden
(SIDA) imeendesha warsha katika Chuo Kikuu cha Ardhi jijini Dar es Salaam na
Chuo cha Ardhi mjiji Morogoro iliyohusu ushirikishwaji wa wananchi hasa makundi
maalum katika upangaji, usimamizi na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya
ardhi nchini.
Katika warsha
iliyofanyika Chuo Kikuu Ardhi na kuhudhuriwa na Wakufunzi pamoja na Wanafunzi
wa chuo hicho, wawezeshaji walikuwa ni Mkurugenzi Mkuu wa Tume Dkt. Stephen
Nindi; Bw. Kent Nillson kutoka Taasisi ya Lantmateriet na Bi. Lilian Looloitai
kutoka Shirika Lisilo la Kiserikali la CORDS ambalo hufanya kazi zake katika
Wilaya za Monduli na Longido Mkoani Arusha.
Akitoa mada katika
warsha hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume alielezea namna gani Sheria, na miongozo
mbalimbali inayohusu upangaji wa matumzi ya ardhi inavyotambua na kuhimiza
ushirikishwaji wa wananchi na kutaja makandi maalum kama vile wanawake kupewa
kipaumbele katika hatua zote za upangaji na utekelezaji wa mipango ya matumizi
ya ardhi. Pia, Dkt. Nindi alitolea mfano wa Mwongozo Shirikishi wa Upangaji wa
Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji (Participatory Land Use Management
Guidelines) ambao umetamka bayana juu ya uundwaji wa kamati za upangaji na
usimamizi wa mipango ya matumizi ya ardhi za vijiji kuwa lazima ziwe na wajumbe
wanawake wasiopungua watatu.
Wakielezea uzoefu wao
juu ya ushirikishwaji katika upangaji wa matumizi ya ardhi, Bw. Kent Nillson
kutoka Taasisi ya Lantmateriet amesema kuwa Sweden ilianza kupangwa toka mwaka
1692 ambapo hadi hivi sasa ushiriki wa wananchi katika shughuli za upangaji na
umiliki wa ardhi umeimarika kwa kiasi kikubwa.
Kwa upande wa mwezeshaji
kutoka Asasi ya Kiraia ya CORDS, Bi. Lilian Looloitai amesema kuwa, kwa muda
mrefu sasa CORDS wamejikita katika uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi
katika Wilaya ya Monduli ambapo ushiriki wa wanawake katika zoezi hilo
unaonyesha kufanikiwa. Bi. Lilian amesema kuwa kwa sasa kumekuwepo na
ongezeko la idadi ya wanawake wanaoshiriki na kutoa maoni katika mikutano ya
kijiji pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
Warsha kama hii pia
imefanyika Chuo cha Ardhi mjini Morogoro ambapo imekuwa chachu ya majadiliano
juu ya upangaji wa mipango ya matumizi ya ardhi kwa njia ya ushirikishwaji
pamoja na kuwaandaa wanafunzi kwa ajili ya kusimamia sekta ya ardhi kwa kuzingatia
masilahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
0 comments:
Post a Comment