METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, February 14, 2019

VALENTINE DAY IMEGEUKA KUWA SIKU YA UZINIFU...!


Na Mathias Canal

Ndugu zangu, Dunia nzima leo imetolea macho Siku ya wapendanao (Valentine Day) ambayo huadhimishwa kila ifikapo tarehe 14 Februari ya kila Mwaka.

Kwenye mitandao ya kijamii inaelekeza kuwa Valentine Day imeanza karne ya 3 huko Roma ambapo alikuwapo padri aliyejulikana kwa jina la St Valentinus aliyekuwa akiishi katika mji wa Roma wakati wa utawala wa Claudis II.

Hata hivyo historia inaeleza kuwa Claudis alitaka awe na jeshi kubwa huku akiamini kwa asilimia 100 kuwa vijana wangejitolea kwa hali na mali na kujiunga na jeshi lake jambo ambalo lilikuwa gumu kidogo kwa vijana hao ambao hawakupenda vita kwa kuogopa kama wangefia vitani maana yake familia zao zingebaki na ukiwa mkubwa.

Pamoja na hayo Claudis alipiga marufuku kwa watu kuoana kwa kuamini kwamba amekosa vijana wengi kwenye jeshi kwa sababu ya ndoa zao imani ambayo pengine haikumsaidia kwani Askofu Valentine naye alikuwa anawafungisha ndoa kwa siri vijana hao.

Claudis aliposikia kuhusu habari hizo za watu kufungishwa ndoa kwa siri aliamuru Askofu Valentine akamatwe ambapo alihukumiwa adhabu adimu kabisa kutokea ya Kifo cha kunyongwa.

Wakati akiwa jela Askofu Valentine alitembelewa mara kwa mara na vijana mbalimbali ambao wao walikwenda kumsalimu huku wakimpatia zawadi ya maua kuonyesha namna ambavyo walimthamini na kumjali na kuonyesha wazi kuwa walikuwa pamoja nae. 

Mmoja kati ya vijana hao waliomtembelea alikuwa ni mtoto wa mkuu wa gereza ambaye yeye aliruhusiwa kuingia hadi Selo pasipo kupingwa kama vijana wengine.

Wakati huo akiwa gerezani huku akisubiri kunyongwa Valentine aliingia kwenye dimbwi la mapenzi dhidi ya binti huyo ambaye ni mtoto wa mkuu wa gereza.

Hata hivyo muda mchache kabla ya kunyongwa Valentine aliomba apatiwe kalamu na karatasi ili aandike ujumbe wake wa kuaga ikiwa ni pamoja na kuweka sahihi yake. Ambapo aliandika "From Your Valentine" (yaani Kutoka kwa Valentine wako) 

Lakini siku ilikuwa imewadia pasina shaka Valentine alinyongwa mpaka kufa tarehe 14 Februari Mwaka 269 BC ambapo baada ya kunyongwa vijana wa Roma walianza kumuiga Valentine kwa kuwaandikia na kuwatumia wanawake waliowapenda salamu za mapenzi.

Kuanzia siku hiyo Tarehe hiyo ikaanza kuhusishwa zaidi urafiki, upendo na mahaba huku ikihusishwa zaidi na mapenzi. Lakini kadri siku zinavyokwenda siku hiyo imezidi kuwa maarufu huku makampuni yakigeuza siku hiyo kuwa ya biashara zaidi kwa kufanya kila kitu maalumu kwa siku ya wapendanao kiwe na muonekana wa rangi yekundu kuanzia kadi za salamu, maua, mpaka nguo wavaazo wapendanao inabidi ziwe nyekundu.

My Take...!

Nimeanza na historia ya Valentine kwa sababu kuu mbili kwanza kuwafanya watu watambue kwanini wanasherehekea siku hii na ina umuhimu gani kwao lakini pili kuwafanya watu watambue kuwa dhana ya Valentine imepotoshwa kimaana.

Kwanza Valentine ni sherehe ya pili kwa umaarufu Duniani ukilinganisha na sherehe ya Krisimasi ambayo ndiyo inatajwa kuwa nafasi ya kwanza kwa umaarufu Duniani, hivyo umaarufu huu unachagizwa na watu ambao ni wavivu katika kutafsiri mambo.

Lakini inawezekanaje kumchukia mtu ndani ya siku 365 halafu ukampenda kwa siku moja pekee...? Inawezekanaje kumpenda mtu kuhusiane na rangi nyekundu ya nguo...? 

Inawezekanaje kuamua kuadhimisha siku ya wapendanao halafu ukajifungia chumbani na mpenzi wako kufanya uzinzi sasa itakuwa siku ya wapendanao ama siku ya mapenzi.

Siku hii tunaitumia vibaya sana tofauti na maana yaani leo hii mpenzi wako usipomwambia Happy Valentine Day anahisi humpendi kwa kuwa ndivyo tulivyojiingiza kwenye maana isiyo yenyewe.

Leo ndio siku ambapo dunia inashangaza kwani ni siku ambayo Nyumba za kulala wageni zitajaa wapenzi, leo ndio siku ambayo watu wanaanzisha mahusiano mapya ya kingono, leo ndio siku ambayo Condom zitanunuliwa kuliko siku zingine zozote zile, Zaidi leo ni siku ambayo kadi zitauzika kuliko siku nyingine huku Club na Bar zikiuza zaidi.

Huu ni ulimbukeni wa kufikiri yaaani siku 365 unamchukia mtu halafu unakuja kujinasibu kwa mapenzi ya saa 24 hii ni dhambi kubwa sana isiyo na kifani japo kwa mujibu wa dini ya kikristo dhambi zote ni sawa.

Binafsi siku zote huwa ninawapenda ndugu, jamaa na Rafiki zangu hakuna siku moja pekee ya kuwapenda.Lakini napenda zaidi watu wapendane kwa moyo wa dhati sio kwa maigizo na ngono zembe.

Tusiangamie kwa kukosa Maarifa, kama tunaadhimisha kumbukizi ya kufa kwa Padri Valentine basi kumbukizi yetu iwe na tafakuri Chanya.

HAPPY VALENTINE'S DAY 
Ni Neno La Wakati Mwema
Mathias Canal
0756413465
Ujiji-Kigoma
Share:

1 comment:

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com