Na Mathias Canal
Ndugu zangu, Dunia nzima leo
imetolea macho Siku ya wapendanao (Valentine Day) ambayo huadhimishwa kila
ifikapo tarehe 14 Februari ya kila Mwaka.
Kwenye mitandao ya kijamii
inaelekeza kuwa Valentine Day imeanza karne ya 3 huko Roma ambapo alikuwapo
padri aliyejulikana kwa jina la St Valentinus aliyekuwa akiishi katika mji wa
Roma wakati wa utawala wa Claudis II.
Hata hivyo historia inaeleza kuwa Claudis
alitaka awe na jeshi kubwa huku akiamini kwa asilimia 100 kuwa vijana
wangejitolea kwa hali na mali na kujiunga na jeshi lake jambo ambalo lilikuwa
gumu kidogo kwa vijana hao ambao hawakupenda vita kwa kuogopa kama wangefia
vitani maana yake familia zao zingebaki na ukiwa mkubwa.
Pamoja na hayo Claudis alipiga
marufuku kwa watu kuoana kwa kuamini kwamba amekosa vijana wengi kwenye jeshi
kwa sababu ya ndoa zao imani ambayo pengine haikumsaidia kwani Askofu Valentine
naye alikuwa anawafungisha ndoa kwa siri vijana hao.
Claudis aliposikia kuhusu habari
hizo za watu kufungishwa ndoa kwa siri aliamuru Askofu Valentine akamatwe
ambapo alihukumiwa adhabu adimu kabisa kutokea ya Kifo cha kunyongwa.
Wakati akiwa jela Askofu Valentine
alitembelewa mara kwa mara na vijana mbalimbali ambao wao walikwenda kumsalimu
huku wakimpatia zawadi ya maua kuonyesha namna ambavyo walimthamini na kumjali
na kuonyesha wazi kuwa walikuwa pamoja nae.
Mmoja kati ya vijana hao
waliomtembelea alikuwa ni mtoto wa mkuu wa gereza ambaye yeye aliruhusiwa
kuingia hadi Selo pasipo kupingwa kama vijana wengine.
Wakati huo akiwa gerezani huku
akisubiri kunyongwa Valentine aliingia kwenye dimbwi la mapenzi dhidi ya binti
huyo ambaye ni mtoto wa mkuu wa gereza.
Hata hivyo muda mchache kabla ya
kunyongwa Valentine aliomba apatiwe kalamu na karatasi ili aandike ujumbe wake
wa kuaga ikiwa ni pamoja na kuweka sahihi yake. Ambapo aliandika "From
Your Valentine" (yaani Kutoka kwa Valentine wako)
Lakini siku ilikuwa imewadia pasina
shaka Valentine alinyongwa mpaka kufa tarehe 14 Februari Mwaka 269 BC ambapo
baada ya kunyongwa vijana wa Roma walianza kumuiga Valentine kwa kuwaandikia na
kuwatumia wanawake waliowapenda salamu za mapenzi.
Kuanzia siku hiyo Tarehe hiyo
ikaanza kuhusishwa zaidi urafiki, upendo na mahaba huku ikihusishwa zaidi na
mapenzi. Lakini kadri siku zinavyokwenda siku hiyo imezidi kuwa maarufu huku
makampuni yakigeuza siku hiyo kuwa ya biashara zaidi kwa kufanya kila kitu
maalumu kwa siku ya wapendanao kiwe na muonekana wa rangi yekundu kuanzia kadi
za salamu, maua, mpaka nguo wavaazo wapendanao inabidi ziwe nyekundu.
My Take...!
Nimeanza na historia ya Valentine
kwa sababu kuu mbili kwanza kuwafanya watu watambue kwanini wanasherehekea siku
hii na ina umuhimu gani kwao lakini pili kuwafanya watu watambue kuwa dhana ya
Valentine imepotoshwa kimaana.
Kwanza Valentine ni sherehe ya pili
kwa umaarufu Duniani ukilinganisha na sherehe ya Krisimasi ambayo ndiyo
inatajwa kuwa nafasi ya kwanza kwa umaarufu Duniani, hivyo umaarufu huu
unachagizwa na watu ambao ni wavivu katika kutafsiri mambo.
Lakini inawezekanaje kumchukia mtu
ndani ya siku 365 halafu ukampenda kwa siku moja pekee...? Inawezekanaje
kumpenda mtu kuhusiane na rangi nyekundu ya nguo...?
Inawezekanaje kuamua kuadhimisha
siku ya wapendanao halafu ukajifungia chumbani na mpenzi wako kufanya uzinzi
sasa itakuwa siku ya wapendanao ama siku ya mapenzi.
Siku hii tunaitumia vibaya sana
tofauti na maana yaani leo hii mpenzi wako usipomwambia Happy Valentine Day
anahisi humpendi kwa kuwa ndivyo tulivyojiingiza kwenye maana isiyo yenyewe.
Leo ndio siku ambapo dunia
inashangaza kwani ni siku ambayo Nyumba za kulala wageni zitajaa wapenzi, leo
ndio siku ambayo watu wanaanzisha mahusiano mapya ya kingono, leo ndio siku
ambayo Condom zitanunuliwa kuliko siku zingine zozote zile, Zaidi leo ni siku
ambayo kadi zitauzika kuliko siku nyingine huku Club na Bar zikiuza zaidi.
Huu ni ulimbukeni wa kufikiri
yaaani siku 365 unamchukia mtu halafu unakuja kujinasibu kwa mapenzi ya saa 24
hii ni dhambi kubwa sana isiyo na kifani japo kwa mujibu wa dini ya kikristo
dhambi zote ni sawa.
Binafsi siku zote huwa ninawapenda
ndugu, jamaa na Rafiki zangu hakuna siku moja pekee ya kuwapenda.Lakini napenda
zaidi watu wapendane kwa moyo wa dhati sio kwa maigizo na ngono zembe.
Tusiangamie kwa kukosa Maarifa,
kama tunaadhimisha kumbukizi ya kufa kwa Padri Valentine basi kumbukizi yetu
iwe na tafakuri Chanya.
HAPPY VALENTINE'S DAY
Ni Neno La Wakati Mwema
Mathias Canal
0756413465
Ujiji-Kigoma
Very nice
ReplyDelete