Maafisa viungo wa Afya moja kutoka Wizara, Idara, Taasisi, Mashirika ya serikali na ya Kimataifa, wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa warsha ya Uongozi wa maafisa viungo wa Afya moja mjini Morogoro leo tarehe 26, Februari, 2019,
Na. OWM DODOMA
Afya Moja ni dhana inayojumuisha
sekta ya afya ya binadamu , wanyamapori, mifugo na mazingira katika
kujiandaa, kufuatilia na kukabili magonjwa yanayoathiri binadamu ,wanyamapori
na mifugo.
Kwa kutambua umuhimu wa
Afya moja nchini, sekta za Afya zenye kujumuisha wataalam wa sekta ya
Afya ya binadamu, Afya ya wanyamapori na mifugo pamoja na mazingira wametakiwa kuanza kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia dhana
hiyo ili uimarishaji wa Afya ya binadamu uwe wa Ufanisi na matokeo bora.
Akiongea wakati wa warsha ya
maafisa viungo wa Afya moja kutoka Wizara, Idara, Taasisi, Mashirika
ya serikali na ya Kimataifa, mjini Morogoro leo tarehe 26, Februari, 2019,
Mkurugenzi Idara ya Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Matamwe Jimmy,
amefafanua kuwa tayari wataalamu hao wanao Mkakati wa kuzileta pamoja
Sekta za Afya kwa ajili ya kuzuia, kukinga na kuthibiti madhara na
magonjwa yanayoikumba nchi yetu, yaani magonjwa ambukizi kati ya wanyama na
binadamu pamoja na usugu wa vimelea vya magonjwa hivyo ni wakati wa kutekeleza
mkakati huo kwa kuitumia dhana ya Afya moja.
“Ninaamini kwamba, wote mnafahamu
kuhusu tishio kubwa la magonjwa kama vile homa ya bonde la ufa, kwenye nchi za
Afrika Mashariki , virusi vya Ebola Afrika Magharibi, kusambaa kwa kiasi
kikubwa cha ugonjwa wa mafua ndege, (HPAI), matatizo ya kupumua
yanayosababishwa na virusi vya Corona, mlipuko wa homa ya Lassa huko Africa
Magharibi na homa ya Zika huko Amerika ya Kusini, kwa hiyo mifano michache
magonjwa hayo yamekuwa tishio kubwa kwa afya ya binadamu na wanyama duniani
kote.” Amesisitiza Kanali Matamwe.
Wakiongea wakati wa warsha hiyo
wataalamu wa sekta za Afya hizo wamebainisha kuwa tayari wamekubaliana
mfumo wa kutoa taarifa na kuhuisha utekelezaji wa mpango mkakati wa afya moja
nchini.
Tarehe
13 Februari 2018, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Kassim Majaliwa alizindua Dawati la Uratibu la Afya moja chini ya Ofisi ya Waziri
Mkuu, likiwa na lengo la kusimamia na kuratibu shughui za Afya moja
nchini. Kwa kutambua umuhimu huo Idara ya Uratibu Maafa Ofisi ya
Waziri Mkuu, kupitia Dawati la Uratibu wa Afya moja kwa kushirikiana
na USAID na Chemonics Internationalwameandaa mkutano wataalam hao.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment