Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Wenye Ulemavu, Mhe. Stella Ikupa akisalimiana na Viongozi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa mara baada ya kuwasili ofisini hapo katika ziara yake ya kukagua utekelezaji wa masuala ya watu wenye Ulemavu Mkoa wa Dodoma.
Mkuu wa mkoa wa Dodoma Mhe. Dkt. Bilinith Mahenge akimweleza jambo Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Wenye Ulemavu, Mhe. Stella Ikupa (Kushoto) jinsi Mkoa wa Dodoma umekuwa ukitekeleza na kuhudumia watu wenye ulemavu.
Baadhi ya washiriki wakisikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye Ulemavu), Mhe. Stella Ikupa (hayupo pichani) wakati wa ziara yake alipokuwa akikagua utekelezaji wa masuala ya watu wenye Ulemavu.
Na; OWM (KVAU) - Dodoma
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu, Mhe. Stella Ikupa ameviasa Vyama vya Watu wenye Ulemavu nchini kuhakikisha wanashirikiana na Serikali katika kuendeleza ustawi wa Watu wenye Ulemavu.
Naibu Waziri Ikupa ameyasema hayo alipofanya ziara Mkoani Dodoma kukagua utekelezaji wa masuala ya Watu wenye Ulemavu ndani ya mkoa huo, ambapo alikutana na viongozi Mkoa na Vyama vya Watu wenye Ulemavu.
Mhe. Ikupa alieleza kuwa ushirikiano baina ya Serikali na vyama vya watu wenye ulemavu ni muhimu katika kuhakisha haki na masilahi ya watu wenye ulemavu yanalidwa kwa kuzingatia Sera, Sheria na Miongozo mbalimbali.
“Serikali imeendelea kuchukua hatua na kutekeleza jukumu lake la kuhamasisha na kuwalinda watu wenye ulemavu nchini kwa kuhakikisha haki za kundi hilo maalumu zinatekelezwa,” alisema Ikupa
Aidha, alisisitiza uongozi wa Mkoa kuhakikisha unahusisha mahitaji maalumu ya wenye ulemavu katika bajeti wanazozitenga, kutoa elimu na taarifa juu ya upatikanaji wa dawa, mafuta ya watu wenye ualbino na vifaa saidizi, na uundwaji wa kamati za kuhudumia wenye ulemavu.
Aliongezea kuwa, ni vyema Maafisa Maendeleo ya Jamii pamoja na maafisa ustawi wa jamii wakahakikisha wanawasaidia watu wenye ulemavu wanapokabiliana na changamoto kwenye uandikaji wa maandiko ya kuomba mikopo.
“Unakuta kikundi cha watu wenye ulemavu wanakuwa wabunifu na wanawazo zuri la kuanzisha mradi au biashara lakini wanakumbana na changamoto ya kuaandaa andiko la miradi yao na hivyo kuwafanya wakate tamaa mapema,” alisema Ikupa
Pia, aliwasii Maafisa Ustawi wa Jamii kuwa na takwimu sahihi za idadi ya watu wenye ulemavu na kuendelea kuweka mifumo mizuri ya kutunza taarifa hizo.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Bw. Edward Mpogolo aliunga mkono na kuyapokea maelekezo yote ya Naibu Waziri na kumhakikishia kuwa Mkoa wa Dodoma utakuwa mstari wa mbele katika kutekeleza maagizo aliyoyatoa.
“Tutafanya kazi kwa ushirikiano mzuri na Vyama vya Watu wenye Ulemavu ili kuangalia namna bora ya kuwahudumia kwa kuzingatia mahitaji yao,” alisema Mpogolo.
Naye Katibu wa SHIVYAWATA Mkoa wa Dodoma, Bw. Justus Ng’wantalima alimpongeza Naibu Waziri kwa jitihada ambazo amekuwa akizifanya katika kutetea Watu wenye Ulemavu.
Katika ziara hiyo Naibu Waziri Ikupa, alitembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Chama cha Walemavu Sulungai kinachojishughulisha na ushonaji wa viatu vya wazi (kobasi) na utengenezaji wa majiko. Vilevile Mhe. Ikupa alitembelea shule ya Viziwi iliyopo Jijini Dodoma.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment