Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi cheti cha kuzaliwa mtoto, Faisal Rashidi
Haroun kabla ya kufungua Mkutano wa Mwaka wa Maafisa Ustawi wa Jamii wa Mikoa
na Halmashauri zote Tanzania Bara, Kwenye ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini
Dodoma, Januari 29, 2019. Kushoto ni Mama Mzazi wa mtoto huyo, Habiba Mohammed.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimpongeza, Fundi Mkuu wa Karakana ya Vifaa Visaidizi vya Wenye Ulemavu iliyopo eneo la Sabasaba jijini Dodoma, Bw. Mwita Marwa Maki baada ya kuvutiwa na baiskeli za magurudumu matatu zilifungwa mota ambazo zimebuniwa na zinatengenezwa na karakana hiyo. Tukio hilo lilifanyika kwenye viwanja vya Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, kabla ya Waziri Mkuu kufungua Mkutano wa Mwaka wa Maafisa Ustawi wa Jamii wa Mikoa na Halmashauri zote Tanzania Bara, Januari 29, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
*Awataka
wajiepushe na rushwa wafanye kazi kwa bidii, weledi na uadilifu
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka Maafisa
Ustawi wa Jamii katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa
watekeleze majukumu yao kwa bidii, weledi, uadilifu na wasijihusishe na vitendo
vya rushwa.
Amesema
maafisa hao wanatakiwa watumie mbinu shirikishi ambazo zinahusisha jamii
yenyewe na wataalamu ambao ni watoa huduma ngazi ya jamii (Community Case
Worker) ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao.
Waziri
Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumanne, Januari 29, 2019) kwenye Mkutano wa
Mwaka wa Kiutendaji wa Maafisa Ustawi wa Jamii katika Sekretarieti za Mikoa na
Mamlaka za Serikali za Mitaa, jijini Dodoma.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu amewataka maafisa hao wahakikishe kwamba haki za msingi za
makundi hayo zinapatikana kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Miongozo iliyopo
katika kutoa huduma ya taaluma yao.
Amesema taaluma
ya Ustawi wa Jamii imepewa dhamana ya kuwa mlinzi wa mtoto, kumhudumia na
kusimamia haki zake, hivyo amewatakawazuie na watokomeze aina zote za
ukatili kwa watoto, wazee na wenye ulemavu.
Waziri
Mkuu amesema jukumu hilo pia linahusisha watoto waliopo kwenye mazingira
hatarishi na wanaoishi na kufanya kazi mitaani, wazee, wanawake wasio na uwezo
na watu wenye ulemavu.
Amesema
pamoja na mafanikio makubwa ambayo Serikali ya Awamu ya Tano imeyapata ni
muhimu wakaendelea kuongeza nguvu na weledi ili kutorudi nyuma katika kujenga
msingi wa kuimarisha ustawi wa makundi maalumu.
Pia,
Waziri Mkuu amewaagiza maafisa hao wakasimamie utekelezaji wa mkakati
wa Mkono kwa Mkono, Familia kwa Familia, Kaya kwa Kaya kupitia huduma
ya kuzuia ukatili ngazi ya familia wenye lengo la kuzuia ukatili ndani ya
familia ili ulete matokeo tarajiwa.
“Tambueni
umuhimu wenu na kwamba jamii inawategemea kutekeleza majukumu yenu kikamilifu
ili kupunguza matatizo ya kijamii kwa wale wenye uhitaji wakiwemo watoto, watu
wenye ulemavu, wazee, familia zenye migogoro na akina mama wanaonyanyaswa na
makundi mengine.”
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amewashukuru wadau wa
maendeleo kwa namna wanavyoshirikiana na Serikali katika kusukuma mbele
gurudumu la maendeleo likiwemo suala la uimarishaji wa huduma za ustawi wa
jamii nchini.
Amesema
anatambua mchango mkubwa kutoka kwa shirika la UNICEF, USAID, UN WOMEN, UNFPA,
John Snow Inc, Pact, HelpAge International, World Vision, Save the Children,
Plan International na wengine wote ambao kwa namna moja au nyingine wameendelea
kushirikiana na Serikali kuinua kiwango cha utoaji huduma za ustawi wa jamii
nchini.
“Ninapenda
kuwahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt.
John Magufuli, ipo tayari kufanya kazi pamoja nanyi ili tuweze kufikia malengo
ya maendeleo endelevu ifikapo 2030.”
Kauli
mbiu ya mkutano wa mwaka huu ni “Uadilifu, Weledi na Uwajibikaji katika Utoaji
wa Huduma za Ustawi wa Jamii Ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa ni Nguzo
katika kuelekea Uchumi wa Kati wa Viwanda.”
Waziri
Mkuu amepongeza kwa kuanzisha utamaduni huo wa kukutana Watendaji wa Sekta ya
Ustawi wa Jamii kwa kuwa hiko ni kiashiria kwamba kuna mabadiliko katika
utendaji kwa kuzingatia kuwa mkutano huu haujawahi kufanyika toka mwaka 2006.
Mkutano
huo wa siku tatu unajumuisha Maafisa Ustawi wa Jamii 164 kutoka mikoa yote
Tanzania Bara, wadau wa maendeleo, wawakilishi wa wazee, watoto waishio katika
mazingira hatarishi waliohitimu mafunzo ya VETA pamoja na watoto waliokuwa
wakiishi mitaani ambao kwa sasa wameunda kikundi cha burudani.
0 comments:
Post a Comment