Waziri wa Madini Doto Biteko
(katikati) akieleza jambo wakati wa kikao cha Menejimenti ya Wizara na Taasisi
zake. Kulia ni Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo na kushoto ni Katibu
Mkuu wa Wizara, Prof. Simon Msanjila.
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus
Nyongo akizungumza jambo wakati wa kikao hicho.
Baadhi ya Watendaji wa Wizara na
Taasisi wakifuatilia kikao hicho
Ø Awataka watumishi kufanyia kazi
maagizo ya Rais Magufuli
Ø Amshukuru Waziri Kairuki kuwa,
amemfundisha Mengi
Ø Aitaka STAMICO kuanza kutoa gawio
kwa Serikali
Waziri
wa Madini Doto Biteko amekutana na Menejimenti ya Wizara ya Madini, Taasisi zake
pamoja na Wenyeviti wa Tume ya Madini na Bodi ya Shirika la Madini la Taifa
(STAMICO), jijini Dodoma, katika kikao ambacho pia kimejadili namna ya
kutekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli
aliyoyatoa wakati akimwapisha Waziri Biteko kushika wadhifa huo Januari 9, 2019.
Biteko
amewataka watumishi wa Wizara na Taasisi
zake ambao hawayajayasikiliza maagizo yaliyotolewa na Rais Magufuli kuhakikisha
kuwa wanayasikiliza ili kuweka uelewa wa pamoja na kushirikiana katika
kutekeleza majukumu ya wizara kwa lengo
la kuhakikisha kwamba sekta ya madini inaimarika.
“ Tuliulizwa dhahabu inauzwa wapi? Basi tusisubiri
tena Rais atuulize inauzwa wapi,” amesisitiza Biteko.
Aidha,
amesisitiza kuwepo kwa ushirikiano wa pamoja miongoni mwa watumishi wa wizara
katika utekelezaji wa majukumu hayo na kusisitiza kuhusu mabadiliko yanayoonekana
kupitia sekta ya madini ikiwemo kufanya kazi na kuongeza kuwa, “
Kinachotuunganisha mahali hapa ni kazi na wala si dini ama jambo lingine,”.
Ameongeza
kuwa, kiu kubwa ya Rais Magufuli ni kuona kuwa watanzania wote wananufaika na
rasilimali madini huku akisisitiza kuwa, kiu yake binafsi ni kuona taswira
nzuri inajengeka kuhusu sekta hiyo ikiwemo kufanya kazi kwa weledi na kuongeza
kuwa, matokeo bado hayaonekani.
“Vipaji
mlivyonavyo mvitumie vizuri vitoe matokeo yanayoonekana. Fanyeni kazi ambazo zitaacha
matokeo yatakayo dumu. Natamani ningezungumza na watumishi wote ili kila mmoja
aelewe kile ninachosema,” amesisistiza Biteko.
Vilevile,
amewataka watendaji kuchukua hatua badala ya kutumia muda mrefu kutafuta
miongozo wakati wanapotekeleza majukumu jambo ambalo linachelewesha utekelezaji
wa majukumu. “ Unasubiri mwongozo gani ilhali unayo Sheria ya Madini?amehoji
Waziri Biteko.
Pia,
amechukua fursa hiyo kumshukuru aliyekuwa Waziri wa Madini Angellah Kairuki na
kueleza kuwa, ni kiongozi ambaye amemfundisha mambo mengi.
“
Namshukuru sana dada yangu, rafiki yangu Angellah. Alinipokea vizuri sana.
Hakuna ushirikiano nilioukosa kwake. Amenifundisha mengi ikiwemo kukaa kwenye
kikao na kujadili mambo kwa kina,” amesema Biteko.
Pamoja
na hayo, Biteko ametumia fursa hiyo kumshukuru Naibu Waziri Nyongo kwa kuwa
naye pamoja katika kipindi chote ambacho alikuwa Naibu Waziri katika wizara ya
madini.
Katika
hatua nyingine, Waziri Biteko ameitaka STAMICO kuhakikisha kuwa, inaanza kutoa
gawio kwa Serikali na ikiwezana, jambo hilo lifanyike kabla ya mwaka ujao wa
fedha.
Kwa
upande wake, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, awali akizungumza katika
kikao hicho, amewataka watumishi ambao hawakupata fursa ya kusikia maagizo ya Rais
Magufuli kufanya hivyo ili kila mmoja asimame kwa lengo moja.
“
Hatukusemwa vizuri. Nchi nzima imesikia na dunia imesikia. Tukiendelea hivi,
hatutavumiliwa,” amesisitiza Nyongo.
Pia,
ameitaka Tume ya Madini kuhakikisha inazingatia na kutekeleza maagizo
yaliyotolewa na Rais Magufuli ikiwemo kutekeleza wajibu wao.
Awali,
akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Profesa Simon
Msanjila amesema kwamba, kikao hicho ni cha kwanza na Waziri Mpya ikiwemo
Mjumbe wa Bodi ya STAMICO na kuongeza kuwa, kinalenga kutoa utambulisho rasmi
wa Waziri Mpya wa Madini na kusikia maelekezo ya Waziri Biteko kufuatia maagizo
yaliyotolewa na Waziri.
Naye,
Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO, Meja Jenerali Mstaafu Michael Isamuhyo
amemweleza Waziri Biteko kuwa, anayapokea majukumu yote yaliyo mbele yake ya
kuhakikisha kwamba shirika hilo linatekeleza majukumu yaliyo mbele yake.
Kikao hicho kimefanyika tarehe 11 Januari,
2019.
0 comments:
Post a Comment