Na Asteria Muhozya, Iringa
Naibu
Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo ameamuru kukamatwa kwa Wamiliki wa mgodi wa
Nyakavangala unaomilikiwa na Thomas
Masuka and Partners kufuatia wamiliki hao
kutofautiana juu ya taarifa waliyoiwasilisha kwa Naibu Waziri kuhusu namna
mgodi huo unavyoendeshwa ikiwemo ulipaji wa kodi na mrabaha wa serikali.
Aidha,
Naibu waziri amewataka wamiliki hao kutoa maelezo ya kina kuhusu ni lini
watalipa kodi zote wanazodaiwa na serikali baada ya kuonekana kuwa mgodi huo
unadaiwa zaidi ya shilingi milioni 128 za mrabaha ambazo imedaiwa kuwa, wapo baadhi
ya wamiliki ambao wamekuwa wakikusanya fedha hizo lakini zimekuwa hazilipwi.
Katika
ziara yake mkoani humo, Naibu Waziri alisema kuwa pamoja na kujionea shughuli
za uchimbaji katika migodi ya dhahabu ya Ulata na Nyakavangala, amebaini
ukwepaji mkubwa wa kodi pamoja na mrabaha wa serikali.
Pia,
amemtaka Afisa Madini kutoa maelekezo ya kina kuhusu suala zima la ulipwaji wa kodi
na mrabaha wa serikali, huku akiagiza zoezi hilo pia limuhusishe Afisa
Msimamizi wa madini aliyekuwepo katika kipindi ambacho fedha hizo hazikulipwa.
“Hatutaki
ugomvi hapa kwenye migodi. Tunataka mgodi ufanye kazi. Dhahabu ziuzwe mahali
panapoonekana. Hapa naona hesabu za viroba tu. Mnunuzi wa dhahabu hapa ni nani”,
alihoji Naibu Waziri.
Wakati
akizungumza na wachimbaji katika mkutano wa hadhara, amewataka wachimbaji hao
kuchimba kwa kuzingatia usalama huku
akisisitiza suala la kufuata sheria na taratibu
huku akiwataka kutoa taarifa za
uhakika kwa wale wote wanaokikuka sheria ikiwemo watoroshaji wa madini
huku akisisitiza utoaji taarifa hizo usiwe wa majungu.
Akitolea
ufafanuzi suala la fedha za mrabaha, amesema fedha hizo hazipaswi kuelekezwa
katika masuala mengine na wamiliki wa migodi ikiwemo kutumiwa katika huduma za
jamii badala yake zinapaswa kulipwa
serikalini.
Naye,
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela aliwataka wamiliki hao kukaa chini na
kukubaliana namna ya kulipa kiasi cha fedha ambacho wanadaiwa na serikali huku
akimtaka Afisa kutoka Halmashauri anayehusika na masuala ya usimamizi wa fedha
kuhakikisha kwamba fedha ambazo mgodi huo ulipaswa kuzilipa kama mrabaha
zinapatikana.
Mgodi
huo wa Nyakavangala unamilikiwa na Thomas Masuka kwa ushirikiano na wawekezaji
wengine wazawa wapatao 20. Wakati akiagiza kukamatwa kwao, wamiliki 8 kati ya
20 ndiyo walikuwa wamehudhuria kikao kati yake na wamiliki hao.
Naibu
Waziri Nyongo alitoa agizo hilo Januari 15 wakat akihitimisha ziara yake ya siku
mbili mkoani humo.
0 comments:
Post a Comment