Na
Priscus Benard – Mpanda Katavi
Kaimu
Mkuu wa Mkoa wa Katavi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Lilian Matinga
amewataka wachimbaji wadogo kuachana na kutafuta
na kuchimba madini kimazoea badala yake wafuate
njia ya kisayansi katika kutafuta, kuchimba na kuchenjua madini katika maeneo
yao ili kuongeza tija, pato lao na Taifa kwa ujumla.
Aliyasema
hayo Disemba 4 wakati wa ufunguzi wa mafunzo
kwa wachimbaji wadogo eneo la D reef na Kapanda Mkaoni Katavi, na kuongeza kuwa, masuala ya madini ni ya
kisayansi na hivyo kuwataka wachimbaji
wadogo kuondoa dhana mbaya iliyojengeka kwa baadhi yao kuwa ukitaka kufanikiwa
katika kuchimba madini unatakiwa uende kwa waganga wa jadi.
Mafunzo
hayo kwa wachimbaji wadogo, yanafuatia utafiti wa kina wa jiosayansi uliofanywa
na wataalam kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kwa kushirikiana na wataalam kutoka Shirika la
Madini la Taifa (STAMICO).
Aliongeza
kuwa, utafiti huo umefanyika
kufuatia nia na azma ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli katika
kuhakikisha kuwa wachimbaji wadogo wanaondokana na uchimbaji usio na tija na
kwenda kwenye uchimbaji utakaoongeza kiwango cha uzalishaji na hivyo kuongeza
kipato kwa wachimbaji na kuboresha maisha yao na jamii kwa ujumla.
“Baada
ya kutumia taarifa za utafiti huu ni matumaini yangu kuwa kipato chenu na
mapato yatokanayo na uchimbaji mdogo wa madini kwa ujumla yataongezeka,”
alisema Matinga.
Pia, Matinga
aliwataka wachimbaji wadogo kuwa wazalendo katika kulipa kodi ili kuunga mkono juhudi
za Rais Dkt. Magufuli katika kuliletea taifa maendeleo makubwa zaidi.
“Miradi
ya maendeleo inahohitaji fedha ni mingi ukianzia elimu bure, mradi wa reli ya
kisasa, bwawa la kuzalisha umeme na mengine mengi,” alisisitiza Matinga.
Awali,
akitoa taarifa ya mazfunzo hayo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa GST, Yokbeth Myumbilwa
alisema utafiti wa kina ulifanyika kwa lengo la kubaini uwepo
na kiasi cha madini, mwelekeo wa miamba, ubora na tabia za mbale katika maeneo
ya D-reef, Kapanda na Ibindi Mkoani Katavi.
Myumbilwa alibainisha kuwa matokeo ya
utafiti huo yanaonesha uwepo
wa mbale za dhahabu kiasi cha tani 4,394,162
zenye wakia 45,773.40
(kilo 1,423.71) za dhahabu
katika eneo la D-reef na tani 452,215
zenye wakia 1,831.92 (kilo 56.98) za
dhahabu katika eneo la Kapanda.
“Matokeo haya ni kwa maeneo ya
D-reef na Kapanda yenye ukubwa wa jumla ya kilomita za mraba 0.06 yaliyofanyiwa
uchorongaji,” alisema Myumbilwa.
Pia,
alieleza kuwa, wataalamu wa GST wapo Mpanda kwa ajili ya kutoa mafunzo
(mrejesho) juu ya matokeo ya utafiti huo. “Kuna watu walifikiri hatutarudi tena
lakini niwahakikishie Serikali ya awamu ya tano ipo pamoja nanyi ndiyo maana
tumerudi hapa kuwapa mafunzo baada ya kukamilika utafiti uliofanyika tokea 2016,”
alisema Myumbilwa.
Vilevile,
alisema kuwa, kupitia mafunzo
hayo yatatoa msukumo katika kuboresha utafutaji, uchenjuaji na uchimbaji salama
na hatimaye kuongeza tija na kipato cha wachimbaji wadogo.
“Wachimbaji
wadogo wanapoteza fedha zao na muda mwingi kwa sababu nyingi ikiwa ni pamoja na
kuchimba kwa kubahatisha na kutokujua njia bora za unjenjuaji madini na hivyo
kupelekea madini yao mengi kupotea kupitia mabaki,” alisisitiza.
Mnamo
Mwaka 2016 Serikali ilitenga kiasi cha dola za kimarekani 3,703,630 kwa ajili
ya utafiti wa kina wa jiosayansi chini ya mradi wa Usimamizi Endelevu wa
Rasilimali Madini (SMMRP) ili kuboresha maisha ya mchimbaji mdogo na kutatua
changamoto zinazomkabili ikiwa ni pamoja na uzalishaji mdogo na uchimbaji
usiozingatia usalama na afya kwa mchimbaji.
Xxxxxxx xxxxxxx
0 comments:
Post a Comment