Mkurugenzi Idara ya Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali, Jimmy
Matamwe akimsikiliza Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kilosa, Asajile
Mwambambale, wakati alipofika ofisini
kwake kwa ajili ya kufuatialia hatua za
menejimenti ya maafa wilayani humo.
Mkurugenzi Idara ya Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali, Jimmy Matamwe akimsikiliza Mratibu wa Maafa wilayani Kilosa Maximillian Ndwangira, akimueleza jinsi tuta la mto mkondoa lilivyoathirika na maji, wakati Mkurugrnzi huyo alipofika wilayani humo shughuli za menejimenti ya maafa.
Wilaya
ya Kilosa imekuwa ikiathiriwa na mafuriko ya mara kwa mara kutokana na mvua nyingi zinazonyesha nchini na
kusababisha kujaa kwa maji katika mito mikubwa inayopita katika wilaya hiyo
ambayo ni mto Mkondoa na Mkundi. Kutokana na hali hiyo Kamati ya Wilaya ya
Usimamizi ya Maafa Kilosa imeliomba Baraza la Taifa la Usimamizi wa Maafa
kuzielekeza wizara za kisekta kukamilisha mpango wa kufufua na kujenga mabwawa
wilayani humo, ili kupunguza kasi ya maji yanayo jaa katika mito hiyo.
Akiongea
wilayani Kilosa wakati wa kufuatilia hatua za urejeshaji hali kutokana na
athari za maafa ya mafuriko yaliyotokana na mvua zilizonyesha, Mkurugenzi Idara
ya Uratibu wa Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali, Jimmy Matamwe ameeleza kuwa
wamelipokea ombi hilo ambalo ni muhimu kutekelezwa kwa ajili ya kupunguza
athari za maafa wilayani humo.
“Mvua
zinaponyesha na tukawa na utaratibu mzuri wa kuyavuna maji hayo, matokeo ya
mvua hizo huwa zinachochea shughuli za maendeleo hasa kilimo, lakini bila
kuyavuna maji yanaweza kusababisha maafa kama
mafuriko. Kwa kulitambua hili, tutaratibu wizara husika kuhakikisha
mabwawa yanafufuliwa ili kuhifadhi maji na kupunguza maji mengi yanayoingia mto
Mkondoa” Alisisitiza Kanali, Matamwe.
Kanali
Matamwe amewataka wananchi wa kilosa kutoendeleza shughuli za kibinadamu kando
ya mto huo kutokana na kuwa serikali imetumia gharama kubwa za kujenga tuta la
mto Mkondoa kwa lengo la kupunguza athari za maafa yaliyokuwa yanatokea baada
ya mto huo kujaa.
Naye
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, ambaye pia ni mwenyekiti
wa Kamati ya Wilaya ya Maafa Bw. Asajile Mwambambale, amefafanua kuwa ipo haja
ya kuharakisha ujenzi wa bwawa la Kidete
ili kuweza kupunguza kasi ya maji ma wingi wa maji yanayo ingia mto Mkondoa,
ambapo athari zake za mafuriko huathiri
watu, mali na miundombinu ya Kilosa.
“Pamoja
na kuwa tungependa utafiti wa kina ufanyike kuanzia kwenye chanzo cha mto
Mkondoa ili kuweza kuelewa tabia ya mto huu, niliombe Baraza la Taifa la
Usimamizi wa maafa, litusaidie kuzielekeza hizi wizara za kisekta, ikiwemo wizara
ya maji, zikamilishe mipango ya kufufua
na kujenga mabwawa ambayo yatasaidia kuhifadhi maji na kupunguza wingi
wa maji yanaoyoingia katika mto Mkondoa” alisema Mwambambale.
Mwambambale
amefafanua kuwa wilaya ya kilosa imeendelea kutekeleza mpango wa Kujiandaa na
Kukabiliana na mafuriko kwa kutoa mchanga kwenye mto Mkondoana Mkundi, ili
kuongeza kina cha mito hiyo. Pia zoezi la Upandaji wa miti na matete kando
ya mto Mkondoa limefanyika. Aidha Kamati
za maafa za kata na vijiji pamoja na timu za uokoaji na kutoa misaada kwa
waathirika wakati wa maafa zimejengewa uwezo.
Wilaya ya Kilosa ni miongoni mwa
wilaya 7 za mkoa wa Morogoro ambayo imekuwa ikiathiriwa na mafuriko ya mara kwa
mara kutokana na mvua zinazonyesha mikoa ya jirani ya Dodoma na Manyara
hususani Wilaya za Mpwapwa, Kongwa na Kiteto, maji ya mvua hizo hupita wilayani
Kilosa kupitia mto Mkondoa na Mkundi.
0 comments:
Post a Comment